Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sudan Kusini ya miezi mitano iliyopita ni tofauti na ya sasa-Shearer

David Shearer, Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini akihutubia waandishi habari jijini New York, Marekani.
UN Photo/Eskinder Debebe)
David Shearer, Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini akihutubia waandishi habari jijini New York, Marekani.

Sudan Kusini ya miezi mitano iliyopita ni tofauti na ya sasa-Shearer

Amani na Usalama

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na mkuu wa Ujumbe wa Umoja huo, nchini Sudan Kusini, UNMISS, David Shearer amesema nchi hiyo ina fursa kubwa ya kusonga mbele iwapo mwenendo wa mchakato wa amani nchini utazingatiwa.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini New York, Marekani Bwana Shearer amesema makubaliano ya amani yaliyofikiwa Septemba mwaka jana kati ya pande mbili husika kwenye mzozo wa Sudan Kusini yamezaa matunda. Ambapo wengi wa wanachama wa upinzani walikuwa Juba na walishiriki mchakato wa amani na kuongeza kuwa mikutano mingi ya amani imekuwa ikiratibiwa na UNMISS kote nchini.

Mkuu huyo wa UNMISS ameongeza kuwa mapigano yamepungua na kwamba ukatili unaochochewa na siasa umepungua kwa kiasi kikubwa, isipokuwa maeneo ya kusini mwa nchi. Amesema baadhi ya watu waliokuwa wamefurushwa wamerejea nyumbani na wengine wameelezea nia yao ya kutaka kurudi. Huku akihsistiza kuwa mafanikio ya mchakato wa amani yatapimwa kwa idadi ya watu watakaorejea nyumbani.

David Shearer, mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Sudan Kusini akutana na wakazi wa Akobo
Picha ya UNMISS/Amanda Voisard
David Shearer, mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Sudan Kusini akutana na wakazi wa Akobo

Hatahivyo, mwakilishi huyo maalum ameelezea wasiwasi wake kuwa kasi ya utekelezaji wa makubaliano ya amani huenda ikapungua kwani mikutano mingi hukosa matumaini ya matokeo. Amesema mikutano yake na wanachama wa baraza la usalama inalenga kuhakikisha amani na kwamba, “ni muhimu tuongee kwa sauti moja, tuunge mkono mchakato wa amani kwani kuna mchakato mmoja tu wa amani, na ni huu, na tujikite katika kuhakikisha kasi na kusongesha mchakato mbele. Iwapo tukifanya hivyo basi Sudan Kusini ina fursa ya kusonga mbele. Nikiangalia nyuma miezi minne au mitano iliyopita ningesema uwezekano wa kuwa mahali tulipo sasa hauwezekani. Na kile ambacho ningependa kufikiria kwa leo ni kwamba katika kipindi cha miezi mitano ijayo, tutakuwa pahali pazuri kuliko tulipo leo katika safari hii ya barabara chanya”.

Akizungumzia tofauti ya makubaliano ya 2015 na ya sasa, bwana Shearer amesema wakati huo pande zote walikuwa na wasiwasi kuhusu wale waliokuwa wamekubaliana na kuongeza kuwa majadiliano ya hivi majuzi yalitoa fursa kwa pande mbili kukubaliana kuhusu mfumo wa hatua za kusonga mbele.Aidha serikali inasimamia sehemu kubwa na kulikuwa na msukumo wa amani  kutoka pande zote mbili.

Bwana Shearere anakubali kuwa, “kuna masuala tata ambayo yanahitaji kusuluhishwa, na hakuna makubaliano ya amani ambayo hayana doa, lakini ni makubaliano ambayo yanatao fursa ya kusongesha mbele Sudan Kusini katika njia muafaka, kando na kuwa tunatambua changamoto ambazo huenda zikatukabili lakini tunamatumani kuwa pande mbili zimedhamiria kuzingatia makubaliano na iwapo hilo litafanyika italeta mabadiliko makubwa nchini Sudan Kusini.”