Mnaohasimiana Sudan Kusini heshimuni makubaliano kati yenu- UN

19 Septemba 2018

Umoja wa Mataifa umezitaka pande kinzani nchini Sudan Kusini ziheshimu makubaliano mapya ya kusitisha mapigano ambayo pande hizo zilitia saini hivi karibuni ili kumaliza mapigano yaliyogubika nchi hiyo tangu mwezi disemba mwaka 2013. Assumpta Massoi na ripoti kamili.

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa MAtaifa nchini Sudan Kusini, David Shearer, amesema hayo leo kwenye mji mkuu Juba wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Alikuwa akigusia makubaliano  hayo ya kusitisha mapigaon yaliyotiwa saini kati ya Rais Salva Kiir na makamu wake wa zamani wa rais Riek Machar akisema Umoja wa Mataifa  unataka kuona ushahidi bayana kuwa pande zote zina utashi wa kisiasa kukomesha ghasia. Hata hivyo amesema..

(Sauti ya David Shearer)

“ Kwa sasa kuna kiungo muhimu kinachokosekana,  nacho ni kuaminiana. Waliotia saini katika makubaliano hayo  zamani walikuwa marafiki na kisha wakageuka kuwa maadui . Kutokana na mazungumzo yangu nao bado kila upande unaushuku mwingine. Kwa hivyo inahitajika kufanya kazi kubwa waweze kuaminiana kati yao na pia na kati ya pande hizo na watu wa Sudan Kusini. Na tunahitaji kushirikiana kwa hilo.”

UNMISS
Walinda amani wa UN wakiwa katika doria huko juba Sudan Kusini.

Kwa mantiki hiyo Bwana Sheare ambaye pia ni mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS amesema..

(Sauti ya David Shearer)

“Umoja wa Mataifa  uko tayari kusaidia utekelezaji wa makubaliano hayo, lakini lazima kuwepo na ratiba ya utekelezaji inayokubalika na pande zote kuweza kufikia hilo.”

Amezikumbusha pande zote husika kwenye makubaliano hayo kuwa mkataba ulitaka mapigano  yasitishwe ndani ya saa 72 tangu kutiwa saini, lakini hadi sasa ingawa kiwango cha mapigano kimepungua bado kuna ripoti za mapigano ya hapa na pale.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud