Hali katika Gaza ni tete, pande zote sitisheni ghasia: Mladenov
Ghasia katika maeneo yanayokaliwa kwa nguvu na Israel kwenye ukingo wa magharibi wa mto Jordan ikiwemo Yerusalem Mashariki zinaongezeka huku mamlaka ya Israel ikiendelea na bomoabomoa na kuchukua kwa nguvu nyumba za wapalestina.
Akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hii leo kwa njia ya video, mratibu maalum wa umoja huo kwenye mchakato wa amani huko Mashariki ya Kati Nickolay Mladenov amesema bomoa bomoa hiyo inayofanywa na Israel si halali hivyo ameiomba isitishe mara moja.
Akinukuu takwimu za ubomoaji zilizotolewana ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA, Bwana Mladenov ameorodhesha nyumba zilizobomolewa.
“Majengo 39 yalibomolewa au kuchukuliwa katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa mto Jordan, yakiwemo majengo matano huko Yerusalem Mashariki ambako ghasia zinaongezeka na hivyo kuacha watu 33 bila ya makazi na pia kuathiri maisha ya watu zaidi ya 100.”
Mratibu huyo amesema kuwa ghasia zinazohusiana na ulowezi zinaongezeka akisema kuwa mashambulio 23 yalifanywa na walowezi wa Israel dhidi ya wapalestina na hivyo kusababisha kifo cha mtu mmoja na kuwajeruhi wengine 12 pamoja na kuharibu mali.
Pamoja na kutaja vitendo vinavyofanywa na Israel, mratibu huyo maalum akaangazia pia vile vinavyotekelezwa kutoka upande wa wapalestina.
Mathalani amesema kuwa tarehe 7 mwezi huu mpalestina mmoja alishambulia na kuwaua kwa kuwapiga risasi raia wawili wa Isreal, akiwemo mwanamume mmoja na mwanamke, katika eneo la viwanda la Barkan kwenye Ukingo wa Magharibi wa mtoJordan ambapo mpalestina huyo alikimbia na hadi sasa anasakwa na vikosi vya vya usalama vya Israel.
Halidhalika jana jumatano, wapalestina walivurumisha maroketi mawili kutoka Gaza hadi Israel ambayo nayo ilijibu mashambulizi kwa kurusha makombora 45 kuelekea upande wa palestina.
Bwana Mladenov amesema kwa ujumla hali ni tete ukanda wa Gaza akikumbusha onyo la hivi karibuni la Benki ya Dunia kuhusu uchumi wa Gaza kuwa unaporomoka ambapo kiwango cha watu wasio na ajira ni asilimia 53 na zaidi ya asilimia 70 ni vijana. “Mtu mmoja kati ya wawili huko Gaza ni fukara,” amesema Mladenov.
Ametoa wito kwa Baraza la Usalama pamoja na marafiki wa Israel na Palestina kushirikiana na Umoja wa Mataifa kuzitaka pande zote kuacha hatua ambazo zitaweka hali ambayo italeta madhila kwa wengine wasio na hatia.
Pia amezitaka pande zote kuendelea na makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyoridhiwa mwaka 2014.
Ameyataka makundi yenye silaha kama vile Hamas na mengine kuachana na uchokozi, na mashambuliio ya maroketi na visa vyote vya kiuchokozi dhidi ya Israel.
Na kwa Israel, Mladenov, ameitaka irejeshe huduma za upelekaji wa bidhaa muhimu hadi Gaza na pia kuboresha njia za kusafirishia bidhaa na kwa watu.