UNMISS yafunga safari kufahamu vitisho wapatavyo wakazi wa Yei

6 Agosti 2019

Nchini Sudan Kusini, ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo,  UNMISS umechukua hatua ya kufunga safari na kukutana na jamii hasa kwenye maeneo yenye mzozo ili kuweza kupata simulizi zao kuhusu vitisho ambavyo wanakutana navyo na hatimaye waweze kufahamu hatua mahsusi za kuepusha ghasia. 

Mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba, msafara wa walinda amani wa Umoja wa Mataifa wanaohudumu kwenye ujumbe wa UNMISS ukiondoka alfajiri kuelekea mji wa Yei ambao kila uchao kunaripotiwa ghasia.

Safari yao ya kilometa 155 imewakutanisha na taswira za mashambulizi ya hivi karibuni kutoka vikundi vilivyojihami sambamba na barabara zisizopitika kwa urahisi kutokana na mvua kubwa za hivi karibuni.

Katika msafara huo walikutana na gavana wa jimbo la Yei Emmanuel Anthony Adil ambaye alizungumzia shambulio hilo akisema,  “hebu na wasikie wito wa amani, hususan ulinzi wa raia. Huwezi kulenga raia ambao wako hatarini, mtu ambaye anahangaika kujikimu maisha yake. Aende sokoni na wewe unamlenga. Nadhani hiki ni kitendo cha uoga uliopitiliza. Lakini tumekubaliana hivi karibuni na UNMISS kuwa tutashirikiana ili raia wajisikie salama na waweze kuendelea na shughuli zao barabarani na miji mikubwa jimboni.”

UNMISS inastaajabu kuwa eneo hili lina rutuba na lina uwezo wa kujikwamua kiuchumi lakini cha kusikitisha ni mapigano  yanayoendelea  yanafurumusha watu, lakini kuna matumaini kama asemavyo Luteni Jenerali Shailesh Tinaikar, mkuu wa kikosi cha UNMISS, “jambo chanya ni kwamba wananchi wanarejea. Tunaona wanarejea taratibu vijijini lakini bado vijiji vingi vimesalia vitupu, nyumba ziko tupu. Tunatumai kuwa baada ya muda tutaweza kurejesha usalama na watu watahamasika kurejea kwenye ardhi hii na kuendelea na kazi yao ya kujenga tena maisha yao.”

Uongozi wa eneo hili unakadiria kuwa wakimbizi wapatao 7,000 hivi karibuni wamerejea kutoka nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na Uganda.

Wengi wao wamekuta makazi yao yameporwa na hivyo kulazimika kuishi na jamaa zao, Joyce Kiden ni mwakilishi wa kikundi cha wanawake wa eneo la Lainya ambaye anasema kwamba, “tunataka amani iwepo, hususan kwetu sisi wanawake ambao ndio tunaumia, tunabeba watoto, tunapikia watoto na hakuna shule za watoto. Tunakaa tu bila mpango wowote kwa sababu ya vita.”

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud