Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Raia walilengwa kwa makusudi huko Equatoria Sudan Kusini hata baada ya makubaliano mapya ya amani- Ripoti

Wananchi wakiwa kwenye hafla ya uzinduzi wa kituo kipya cha ulinzi wa aman ihuko Yei nchini Sudan Kusini kufuatia ombi la wakazi wa eneo hilo baada ya ghasia kuanza tena mwezi Januari mwaka huu.
UN /Eric Kanalstein
Wananchi wakiwa kwenye hafla ya uzinduzi wa kituo kipya cha ulinzi wa aman ihuko Yei nchini Sudan Kusini kufuatia ombi la wakazi wa eneo hilo baada ya ghasia kuanza tena mwezi Januari mwaka huu.

Raia walilengwa kwa makusudi huko Equatoria Sudan Kusini hata baada ya makubaliano mapya ya amani- Ripoti

Haki za binadamu

Kipindi cha miezi minane cha makubaliano mapya ya amani nchini Sudan Kusini, kimeshuhudia mauaji  ya zaidi ya raia 100 huko eneo la kati la Equatoria nchini humo huku idadi kama hiyo hiyo ya wasichana na wanawake wakibakwa au kufanyiwa ukatili wa kingono kutokana na mapigano mapya.

Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti mpya ya kitengo cha haki za binadamu cha ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS ambaye imerekodi matukio tofauti 95 ya ukiukwaji wa haki za binadamu tangu mwezi Septemba mwaka jana wa 2018 hadi mwezi Aprili mwaka huu.

“Visa hivyo ni pamoja na mashambulizi 30 kwenye vijiji ambayo yalisababisha vifo vya raia 104 na wengine 35 walijeruhiwa sambamba na kutekwa nyara kwa watu 187,” imesema ripoti hiyo iliyotolewa leo na msemaji wa UNMISS huko Juba, Sudan  Kusini.

Halikadhalika ghasia hizo zilisababisha watu zaidi ya 56,000 kuwa wakimbizi wa ndani nchini Sudan Kusini na takribani wengine 20,000 walivuka mpaka na kukimbilia nchi jirani za Uganda na Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo.

“Hata hivyo kwa ujumla matukio ya ukiukwaji wa haki  yanayohusiana na mapigano yamepungua kufuatia kutiwa saini kwa makubaliano hayo mapya ya amani mwezi Septemba mwaka jana lakini kwa eneo la Equatorai ya Kati, hali imekuwa ni toafuti, hususan maeneo yanayozingira mji wa Yei ambako mapigano yanaendelea,” imesema ripoti hiyo.

Mwanamke akichora kwenye ukuta maandishi yanayosema amani, katika mji wa yei
UNMISS/Denis Louro
Mwanamke akichora kwenye ukuta maandishi yanayosema amani, katika mji wa yei

Je ni nani anahusika na mauaji hayo ya raia?

Ripoti hiyo imetaja makundi matatu yanayoshambulia raia kuwa ni vikundi vilivyojihami ambavyo havikutia saini makubaliano mapya ya amani kama vile National Salvation Front, NAS, Kikudni cha South Sudan National Movement for Change, SSNMC, na  vikundi shirika vilivyojihami vyenye uhusiano na vikosi vya serikali pamoja na kikundi cha SPLA/IO au upande wa upinzani kinachomuunga mkono Riek Machar.

Ghasia hizo zilifanyika katika awamu mbili ambapo awamu ya kwanza ni wakati wa kutiwa saini kwa makubaliano mapya ya amani ambapo vikundi vya SPLA-IO (RM) na vile vya NAS, SSNMC na vingine vilivyojihami vilipambana kuhusu udhibiti wa sehemu ya eneo hilo la kati mwa Equatoria.

Katika awamu hiyo ya kwanza, vikundi hivyo viliwajibika na mauaji ya raia wapatao 61 huku wengine 150 wakishikiliwa wakiwemo wanawake na wasichana ambao walichukuliwa kama wake za makamanda na walibakwa au kupigwa.

Awamu ya pili ya ghasia ilianza mwezi Januari mwaka huu wakati serikali ya Sudan Kusini ilipozindua operesheni ya kijeshi kufurumusha waasi kutoka eneo la kati la Equatoria.

Maelfu ya wakimbizi wa ndani wakiwa wamekusanyika katika eneo la kanisa la Emmanuel huko Yei, Sudan Kusini.
UNHCR/Rocco Nuri
Maelfu ya wakimbizi wa ndani wakiwa wamekusanyika katika eneo la kanisa la Emmanuel huko Yei, Sudan Kusini.

Kinachofanyika baada ya uchunguzi kubaini  ukiukwaji wa haki

Tayari Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amefanya ziara za mara kwa mara kwenye eneo hilo ili kusaka mazungumzo na viongozi wa kisiasa na kijeshi kuhusu masuala ya haki za binadamu yaliyoibuliwa  kwenye ripoti, sambamba na athari za ukimbizi wa ndani na umuhimu wa maridhiano na amani.

Ripoti hiyo imetaka pande zote kwenye mzozo ziheshimu haki za kimataifa za binadamu na haki za kibinadamu ambapo hivi sasa UNMISS inaisihi serikali ya Sudan Kusini izingatie wajibu wake wa msingi wa kulinda raia.

Ripoti hii ilisambazwa mapema kwa serikali na muhtasari wake ulipelekwa kwa pande zote kwenye mzozo wa Sudan Kusini na tayari UNMISS imepokea barua kutoka kwa Machar akitaka makamanda wa SPLA-IO wanaomuunga mkno wachunguze kilichoibuliwe kwenye ripoti ili wahusika wawajibishwe.

Naye kiongozi wa NAS Thomas Cirillo amewasiliana na UNMISS kuhusu masuala yanayomhusu ambayo yamo kwenye ripoti.