Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNMISS yatathimini hali ya Yei Sudan Kusini

Mwanamke akichora kwenye ukuta maandishi yanayosema amani, katika mji wa yei
UNMISS/Denis Louro
Mwanamke akichora kwenye ukuta maandishi yanayosema amani, katika mji wa yei

UNMISS yatathimini hali ya Yei Sudan Kusini

Amani na Usalama

Wakati jitihada za kutekeleza makubaliano ya amani yaliyotiwa saini mnamo mwezi Septemba mwaka 2018 zikiendelea mjini Yei Sudan Kusini, eneo la kilimo ambalo liliwahi kuwa chanzo kikuu cha chakula nchini humo bado linakabiliana na ukikukwaji mkubwa wa haki za binadamu na watu kuyahama makazi yao. 

Siku za hivi karibuni vikosi vya walinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini , UNMISS walikuwa katika eneo hilo ili kutathimini hali ya haki za binadamu . Yei ikiwa imesalia hifadhi kwa watu wachache, maisha yametoweka kabisa katika mji huu ulio katikati ya eneo la biashara ambalo sasa maduka yote yamesalia kufungwa. 

Msichana huyu mwenye umri wa miaka 15 anaeleza hadithi ya ajabu ya kutekwa kwake mnamo mwaka 2016 wakati alipokuwa na umri wa miaka 12.

(Sauti ya msichana)

 “Tulikuwa njiani kutoka Congo na wakamuua kijana wa kiume tuliyekuwa naye karibu na kambi yao, mbele ya macho yetu. Mimi na Bibi yangu tuliachwa. Walikuwa wauaji 15, mmoja wao alitaka kunioa lakini nilikataa kwa hivyo alianza kuninyanyasa. Kwa namna nilivyoteseka pale ni Mungu pekee ajuaye. Hivi sasa ninataka kwenda shule lakini sijui lolote kuhusu wazazi wangu, sasa nitafanya nini? Ni miaka mitatu sasa tangu nilipowapoteza wazazi wangu, nitafanya nini?”

Afisa wa haki za binadamu katika ujumbe wa umoja wa, UNMISS aliyeko Yei anasema wanawasiliana na waathirika kuhakikisha kuwa maisha yao na ustawi wao unalindwa kwanza na pia wanapata huduma za kitabibu.

(Sauti ya Arthur Beingana)

 “Kwa upande wa ufuatiliaji, kuandika na kutoa taarifa, pia tunawahusisha washiriki ili kuhakikisha kwamba wahalifu wanatambuliwa, na wanajibishwa kwa sababu huu ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu ambao hatutakiwi kuuficha chini ya zulia na kwamba wahalifu wanapaswa kuwajibika.”

UNMISS imeongeza doria kwenye maeneo ambayo taarifa za ukiukwaji huo zinaenea.

(Sauti ya Arthur Beingana)

 “Tunafanya doria za aina mbili, zile za umbali mfupi na zile za umbali mrefu ili kuhakikisha kuwa tunaonesha uwepo wetu na kuhakikisha vikosi vyetu vya usalama vinakuwepo katika jamii angalau kunakuwa na upunguzaji wa ukiukwaji wa haki za binadamu.”

Wakati jitihada za kisaiasa zikiendelea ili kurejesha amani kote Sudan Kusini, UNMISS ina matumaini kuwa doria hizi zitazuia kutokea kwa mapigano zaidi dhidi ya wananchi katika eneo la Yei na hivyo kuchangia kurejesha amani katika eneo ambalo lilipata kuwa chanzo cha chakula kwa nchi hiyo.