Watu 150 wakifa maji Mediteranea, UN yasema ‘chonde chonde tuchukue hatua,”

26 Julai 2019

Kufuatia janga la kuzama kwa boti kwenye bahari ya Mediteranea karibu na pwani ya Libya, Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameeleza  masikitiko yake kutokana na vifo sambamba na kushikiliwa korokoroni kwa baadhi ya manusura wa kisa hicho.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limeripoti kuwa kuzama kwa boti hiyo jana kumesababisha watu 150 huku wanawake wajawazito pamoja na watoto wakiwa bado hawajulikani walipo.

Bwana Guterres pia ameelezea wasiwasi wake kuwa manusura  wanaoshikiliwa ni katika kituo cha Tajoura ambacho kipo karibu na kituo cha kijeshi kilichopigwa kwa kombora tarehe pili mwezi huu wa Julai na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 50.

Katibu Mkuu amesisitiza kuwa Libya si nchi salama kwa wasaka hifadhi na kwamba wakimbizi lazima watendewe kiutu, kwa heshima na kwa mujibu wa sheria za kimataifa za kibinadamu.

Akizungumzia tukio hilo la jana, Kamishna Mkuu wa wakimbizi kwenye Umoja wa Mataifa, UNHCR, Filippo Grandi amesema iwapo idadi hiyo ya watu 150 itathibitishwa, basi itakuwa ni tukio la kusababisha vifo vingi zaidi tangu mwezi Mei mwaka 2017.

UNHCR inasema hata kabla ya  tukio la jana, idadi ya vifo vya watu Mediteranea kwa mwaka huu pekee ni 669.

“Tukio baya zaidi kwenye bahari ya Mediteranea ndio limetokea. Kurejesha harakati za uokozi baharini, na kuondokana na ushikiliaji wa wahamiaji na wakimbizi Libya lazima kufanyike haraka kabla hatujachelewa zaidi,” amesema Bwana Grandi.

Kwa mantiki hiyo amesema, “UNHCR inachukua fursa ya sasa kujitokeza kuwa tayari kwa msaada wowote wa ziada, ikiwemo kusaidia harakati za kusaka maeneo ya ziada ya hifadhi salam nje ya Libya.”

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter