Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Libya msiwaweke rumande wahamiaji waliookolewa pwani- IOM

Wahamiaji wakiwa wamelala kwenye magodoro kwenye moja ya vituo vya kushikilia wahamiaji huko nchini Libya.
UNICEF/Alessio Romenzi
Wahamiaji wakiwa wamelala kwenye magodoro kwenye moja ya vituo vya kushikilia wahamiaji huko nchini Libya.

Libya msiwaweke rumande wahamiaji waliookolewa pwani- IOM

Wahamiaji na Wakimbizi

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la uhamiaji la Umoja wa Umoja wa Mataifa IOM, William Lacy Swing amewaomba viongozi wa Libya waache kuwaweka ndani wahamiaji wanaozuiliwa baada ya kukamatwa na walinzi wa pwani wa nchi hiyo wakivuka baharí ya Mediteranea.

Bwana Swing amesema hayo leo mjini Tripoli Libya ambako anazuru kuona hali ya wahamiaji ilivyo na pia kusaka jinsi ya kuwezesha wahamiaji kurejea kwa hiari makazi yao halisia.

Amesema katika mazungumzo yake na waziri mkuu wa Libya, Fayez al-Sarra, amemuomba kuwa wahamiaji wanaorejeshwa pwani au wanaookolewa na walinzihao wa pwani wasiwekwe ndani bali wale wanaotaka kurejea nyumbani kwa hiari mchakato wao uharakishwe badala ya kuwashikilia.

Kwa mujibu wa msemaji wa UNHCR mjini Geneva, Uswisi Leonard Doyle msaada wa Muungano wa Ulaya, EU umewezesha Libya kuongeza kasi ya msako wa usafirishaji haramu binadamu.

Amesema idadi ya wahamiaji ambao wanaokolewa au wanakamatwa na walinzi wa pwani ya Libya wakiwa eneo la maji la nchi hiyo imeongezeka na kufikia 4,000 mwezi uliopita pekee.

 

Picha kutoka video mpya toka kundi la Degg Force 3 kibao kikipatiwa jina la Falé kikieleza uhalisia wa safari ya vijana wawili kuvuka jangwa kusaka hali bora Ulaya.
IOM/Guinea
Picha kutoka video mpya toka kundi la Degg Force 3 kibao kikipatiwa jina la Falé kikieleza uhalisia wa safari ya vijana wawili kuvuka jangwa kusaka hali bora Ulaya.

Baada ya kukamatwa wahamiaji hupelekwa korokoroni ambako kumejaa kupita kiasi, na hofu kubwa ikisalia kuhusu ustawi wao.

Kwa mantiki hiyo Bwana Swing amesema ni matumaini yake kuwa mabadiliko hayo ya kisera yatafanyika kwa kuwa inaonekana ni ukatili kuwarejesha korokoroni wahamiaji waliokuwa wanasaka kwenda Ulaya, hususan kama si lazima kuwaweka ndani.

Balozi Swing amemshukuru pia Waziri Mkuu wa Libya kwa kutafakari pendekezo lake la kuacha kuwazuia wahamiaji na pia kuwatenga wanawake na watoto wanaozuiliwa.