Makubaliano yaliyofikiwa EU kuhusu hali ya Mediteranea yatutia moyo- IOM/UNHCR

23 Julai 2019

Viongozi wa mashirika mawili  ya Umoja wa Mataifa wamekaribisha uamuzi uliofikiwa barani Ulaya wenye lengo la kushughulikia hali wahamiaji na wakimbizi kwenye bahari ya Mediteranea na kuzuia vifo nchini Libya.

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Uhamiaji la Umoja wa Mataifa IOM António Vitorino na lile la kuhudumia wakimbizi, UNHCR Filippo Grandi wamesema hayo kufuatia makubaliano yaliyotokana na mjadala uliofanyika mjini Paris, Ufaransa miongoni mwa mataifa ya Ulaya.

“Tunakabirisha makubaliano ya leo kuhusu umuhimu wa kumaliza ushikiliaji holela wa wakimbizi na wahamiaji nchini Libya. Kuna umuhimu wa kuwepo kwa mchakato halali wa kuachia watu wanaoshikiliwa kwenye vituo iwe mijini au kuwepo kwa maeneo ya wazi ya kuwawezesha kutembea huru na kupata msaada bila kudhurika,” wamesema viongozi hao kupitia taarifa yao ya pamoja.

Viongozi hao wamesema kwa kuzingatia hatari ya kuweza kunyanyaswa, au kuteswa au kufariki duniani, mtu yeyote hapaswi kurejeshwa kwenye vituo wanavyoshikiliwa nchini Libya baada ya kukamatwa au kuokolewa baharini.

Kuhusu hali ya sasa ya mashirika ya kiraia na meli za kibiashara kuachiwa jukumu la operesheni za kusaka na uokozi, Bwana Vitorino na Bwana Grandi wamesema hii haipaswi kuendelea bali mfumoi wa awali wa nchi za Muungano wa Ulaya wa kusaka na uokozi unahitajika.

Hata hivyo wamesema jukumu la mashirika ya kiraia linapaswa kutambuliwa na kwamba yasionekane yanatenda uhalifu au yasinyanyapaliwe kwa kuokoa maisha ya watu baharini.

Wahudumu wa afya wakiwa wamembeba mmoja wa manusura wa tukio la kuzama kwa moja ya vyombo vya majini kwenye bahari ya Mediteranea.
PICHA: UNHCR/F. Malavolta
Wahudumu wa afya wakiwa wamembeba mmoja wa manusura wa tukio la kuzama kwa moja ya vyombo vya majini kwenye bahari ya Mediteranea.

Halikadhalika viongozi hao wa IOM wametiwa moyo na majadiliano ya mataifa hayo ya Muungano wa Ulaya kuhusu kuanzishwa kwa  mfumo wa muda unaotambulika kwa ajli ya watu wanaowasili baada ya kuokolewa baharini na uwajibikaji wa pamoja wa mataifa hayo katika kuwapatia hifadhi watu hao.

Hata hivyo wamesema wakati hayo yanaendelea, uhamishaji na upatiaji wahamiaji na wakimbizi nchi ya tatu kutoka  Libya ni muhimu kwa watu hao ambao sasa wanakabiliwa na vitisho.

“Tunaendelea kusihi mataifa yashirikiane nasi ili kutambua wale wakimbizi walio hatarini zaidi nchiin Libya na tuweze kuwaondoa na tunakaribisha kauli ya usaidizi ambazo zimetolewa hii leo,” wamesema viongozi hao.

Sambamba na hilo wamesisitiza umuhimu wa kupata suluhu ya kudumu kwa mzozo nchini Libya wakisema hicho ni kipaumbele cha juu zaidi wakisihi jumuiya ya kimataifa itumie uwezo wake kuleta pande kinzani pamoja kwa ajili ya mazungumzo ili hatimaye suluhu ya kudumu ipatikane na amani na utulivu virejee.

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter