Mahabusu kwa waoomba hifadhi Libya zisite:UNHCR

23 Novemba 2018

Ikiwa leo ni mwaka mmoja tangu shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR lianze operesheni ya kuokoa maisha ya kuwahamisha kutoka Libya maelfu ya wakimbizi na waoomba hifadhi, jumla ya watu 25000 wameshahamishwa wengi walikuwa mahabusu au kushikiliwa kwenye vituo maalumu.

Kwa mujibu wa shirika hilo wengi wa watu hao wamesafirishwa kwa ndege na kupelekwa Niger, Italia na Romania. Wakimbi zin a waoomba hifadhi walioahamishwa hivi karibuni ni 132 wakijumuisha wanawake na watoto na walisafirishwa kutoka Tripoli jana hadi Niger ambako wanahifadhiwa na mpango wa dharura wa UNHCR wakisubiri kupatiwa suluhu ya muda mrefu ya kupelekwa kwenye nchi ya tatu.

Watu wote waliohamishwa walikuwa wanashikiliwa katika mahabusu za vituo vya trig Al Sikka na Abu salim mjini Tripoli. 41kati yao ni watoto walio peke yao bila wazazi au walezi ambapo wengi walishikiliwa baada kukamatwa au kuokolewa baharini wakijaribu kusafiri kupitia Libya kwenda Ulaya.

Kwa kutambua hatari inayowakabili wakimbizi na wahamiaji nchini Libya, UNHCR halichukulii nchini humo kuwa ni kituo salama cha kupitia na haishauri kuwaresha Libya watu wanaokolewa baharini au wanaokamatwa katika msako.

Roberto Mignone mkuu wa UNHCR nchini Libya amesema “wakimbizi nchini Libya wanakabiliwa na jinamizi kubwa. Wamekimbia nyumba zao kwa kusaka usalama na ulinzi na badala yake wanaishia jela, wakiteseka pasi kikomo kwenye mazingira na hali mbaya.”

Ameongeza kuwa inasikitisha kuona watu hawa wanashikiliwa mahabusu badala ya kulindwa nah ii ni licha ya ukweli kwamba njia mbadala kwa watu hawa Libya inaweza kupatikana badala ya kuwafunga , ikiwemo kupitia kituo cha kuwakusanya na kuwasafirisha ambacho tumekuwa tukisubiri kukifungua tangu Julai. Na kituo hiki kinaweza kutoa ulinzi na usalama mara moja kwa walio walio katika hatari.

Sasa UNHCR imetoa wito kwa serikali ya Libya kusitisha hatua za kuwashikilia katika vituo wakimbizi na waoomba hifadhi hao badala yake kutimiza wajibu wake kwa kuzingatia mikataba na sharia za kimataifa kuhusu wakimbizi na waoomba hifadhi.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter