Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bado nchi zinasuasua kudhibiti matumizi ya tumbaku- Ripoti

Kibao cha kupiga marufuku uvutaji wa sigara kwenye eneo la bustani ya  mboga katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New  York, Marekani.
UN News/Yasmina Guerda
Kibao cha kupiga marufuku uvutaji wa sigara kwenye eneo la bustani ya mboga katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.

Bado nchi zinasuasua kudhibiti matumizi ya tumbaku- Ripoti

Afya

Shirika la afya ulimwenguni, WHO hii leo limetoa ripoti yake kuhusu matumiziya tumbaku duniani inayoonesha kuwa licha ya mafanikio katika kudhibiti  matumizi ya bidhaa hiyo bado kuna changamoto ya utekelezaji wa sera ikiwemo zile za kusaidia watu kuondokana na matumizi ya tumbaku.

Ripoti hiyo ya Saba inayochunguza janga la matumizi ya tumbaku inasema kuwa serikali nyingi zimesonga mbele mara nne zaidi kuliko muongo mmoja uliopita katika kuchukua hatua za kudhibiti.

Hatua hizo ni pamoja na marufuku ya kuvuta tumbaku maeneo ya umma na kuweka michoro ya maonyo kuhusu madhara ya matumizi ya tumbaku kwenye vifungashio vya sigara.

Hata hivyo bado kuna changamoto katika kutekeleza yaliyomo kwenye mkataba wa kimataifa wa kudhibiti matumizi ya tumbaku, FCTC, mambo ambayo yameonesha kusaidia zaidi kuokoa maisha na kuepusha gharama za kiafya zitokanazo na matumizi ya tumbaku.

Mambo hayo sita ambayo yalizinduliwa mwaka 2007 ambayo bado WHO inapigia chepuo ni pamoja na kufuatilia matumizi ya tumbaku na kuweka sera za uzuiaji.

Juhudi za kupunguza matangazo ya Sigara kama haya zinaendelea kote duniani ili kupunguza ufutaji wa sigara ambao una athari mbaya kwa afya ya binadamu na mazingira.
Maggie Murray-Lee
Juhudi za kupunguza matangazo ya Sigara kama haya zinaendelea kote duniani ili kupunguza ufutaji wa sigara ambao una athari mbaya kwa afya ya binadamu na mazingira.

Pili ni kulinda watu dhidi ya moshi wa tumbaku, tatu kusaidia wavutaji kuacha kutumia tumbaku, nne kuweka maonyo kuhusu madhara ya kiafya ya tumbaku na tano, kusimamia udhibiti wa matangazo ya tumbaku na sit ani kuongeza kodi kwenye bidhaa za tumbaku.

Katika wavuti wake, WHO imetaja madhara ya kiafya ya matumizi ya tumbaku kuwa ni saratani  ya mapafu ikisema kuwa, tumbaku ndio chanzo cha theluthi mbili ya vifo vitokanavyo na saratani ya mapafu duniani kote kila mwaka.

Halikadhalika inasema, “uvutaji wa moshi wa tumbaku utokanao na tumbaku aliyovuta mtu mwingine nao  husababisha saratani ya mapafu na kwamba kuacha kuvuta tumbaku kunaweza kupungua saratani ya mapafu. Baada ya miaka 10 ya kuacha kuvuta tumbaku, hatari ya kupata saratani  ya mapafu hupungua kwa asilimia 50.”

WHO inasema pia watoto wanaokumbana na moshi wa tumbaku kupitia tumboni mwa mama zao wanapata shida ya ukuaji wa mapafu yao na kwamba wanapozaliwa, mara kwa mara wanapata magonjwa ya njia ya hewa. “Duniani kote takribani watoto 60,000 hufariki dunia kabla ya kutimiza umri wa miaka 5 kutokana na matatizo ya njia ya hewa yaliyosababishwa na kuvuta moshi wa tumbaku,” imesema WHO.