Mkataba dhidi ya tumbaku umeboresha afya ya umma- WHO
Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya duniani WHO, Dkt Tedros Adhonom Ghebreyesus ameusifu mkataba wa kimataifa wa kudhibiti matumizi ya tumbaku, FCTC, kama moja ya mafanikio makubwa ya afya kwa jamii katika kipindi cha miaka 20 iliyopita.
Dkt. Tedros amesema hayo leo mjini Geneva Uswisi kabla ya kuanza kwa mkutano wa nane nchi wanachama wa mkataba huo, (COP8) , mkutano wenye lengo la kuanisha mwelekeo wa kuimarisha na kupanua wigo wa mkataba huo wa aina yake duniani.
Dkt Tedros amesema kuwa tangu mkataba huo uanze kutumika miaka 13 iliyopita, umesalia kuwa nyaraka muhimu inayotumiwa duniani kuendeleza afya ya jamii.
Amesema kupitia mkataba huo nchi nyingi zimepitisha sheria za kudhibiti matumizi ya tumbaku ikiwemo kuongeza kodi kwa bidhaa za tumbaku, kuweka maeneo salama ambako hairuhusiwi kuvuta sigara na kutaka kuwekwa kwa onyo lenye maandishi makubwa katika bidhaa za tumbaku, mfano sigara.
Katika mkutano huu wa COP8 ambao unajumuisha wajumbe kutoka mataifa 137 wakiwemo wajumbe kutoka mashirika kadhaa ya Umoja wa Mataifa, kutazinduliwa ripoti mpya, iliyopewa jina la , “Ripoti ya WHO kuhusu maendeleo ya utekelezaji wa FCTC duniani,” ambayo inamulika ripoti mbalimbali ambazo ziliwasilishwa na wahusika wa mkataba huo katika kipindi cha mwaka wa 2018.

Ripoti inamulika mafanikio duniani ya kudhibiti matumizi ya tumbaku kutoka katika hatua za kudhibiti na utekelezaji ambao utawezesha kupunguza matumizi ya tumbaku, pamoja na changamoto zilizopo kutokana na mapengo katika será na viwanda vya sigara.
Kikubwa kitakachojadiliwa katika mkutano wa COP8, unaoanza leo hadi tarehe sita Oktoba, ni kuweka mkakati jaribio wa kipindi cha kadiri ambao utaeleza vipaumbele vya kuongeza na kuimarisha ajenda ya kudhibiti tumbaku ulimwenguni na pia kuimarisha utekelezaji wa mkataba hadi kipindi kingine cha miaka mitano.
Hii inahusu miongoni mwa mengine kuona kama juhudi za kudhibiti tumbaku zinahusu pia mwelekeo mpya kuhusu madhara ya bidhaa za tumbaku dhidi ya maendeleo na mazingira.
Mkurugenzi Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Michael Moller, amekariri umuhimu wa kuunganisha udhibiti wa tumbaku na mikakati ya malengo ya maendeleo endelevu akimaanisha kulenga asilimia 80 ya wavutaji sigara duniani bilioni 1.1 ambao huishi katika mataifa yenye kipato cha chini na cha wastani.