Vitamini D haipunguzi hatari ya saratani

27 Aprili 2018

Matumizi ya vitamini D mwilini hayana uhusiano wowote na kupunguza hatari ya binadamu kupata ugonjwa wa saratani ya mapafu.

Hiyo ni kwa mujibu wa utafiti mpya kutoka shirika la kimataifa la utafiti wa saratani, IARC, utafiti ambao unafuta matokeo ya tafiti za awali zilizoonyesha uhusiano kati ya uwepo wa kiwango kikubwa cha Vitamini D mwilini na kupungua kwa hatari ya mtu kupata saratani hiyo.

Vitamin D huzalishwa mwilini baada ya mtu kupata mionzi ya ultraviolet B au (UVB) kutoka kwenye jua au mtu kumeza vidonge vya vitamini hiyo.

Mtafiti mkuu Dkt. Paul Brennan amesema walifanya utafiti wa kina na mpana zaidi kwa kutumia wavuta sigara, walioacha kuvuta na hata kuangazia uwepo wa Vitamin D mwilini na kuhusisha na saratani  ya mapafu.

Matokeo ni kwamba si kweli uwepo wa Vitamini D mwilini unapunguza hatari ya mtu kupata saratani ya mapafu.

Kwa mantiki hiyo watafiti wanasisitiza kinga kuu dhidi ya saratani hiyo ni watu kuacha kuvuta sigara kwa kuwa sababu kuu ya saratani hiyo ni tumbaku.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud