Kenya imepiga hatua Afrika katika nafasi ya ubunifu wa kimataifa-WIPO

Wazungumzaji kati jopo la kimataifa la orodha ya ubunifu duniani mwaka 2019
WIPO/Hemant Chawla
Wazungumzaji kati jopo la kimataifa la orodha ya ubunifu duniani mwaka 2019

Kenya imepiga hatua Afrika katika nafasi ya ubunifu wa kimataifa-WIPO

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Shirika la hakimiliki duniani, WIPO leo limezindua ripoti ya maendeleo na ubunifu kimataifa kwa mwaka 2019 huku ikitaja India kama nchi iliyopiga hatua kubwa zaidi kutoka nafasi ya 81 hadi 52 tangu mwaka 2015, pia nchi zingine tatu ambazo zimetajwa kupiga hatua kubwa katika kipindi cha miaka tisa iliyopita ni Kenya, Viet Nam na Maldives.

Kwa mujibu wa ripoti kwa nchi za Afrika kusini mwa Jangwa la Sahara, nchi ya Afrika Kusini inaongoza katika nafasi ya 63, ikifuatiwa na Kenya 77 na Mauritius katika nafasi ya 82. Akizungumza kufuatia uzinduzi huo, mkurugenzi mkuu wa WIPO, Francis Gurry amesema, “ufuatiliaji wa ubunifu kimataifa, GII umekuwa ni kigezo cha kupima ubunifu na utendaji kimataifa na umuhimu wake ni kufuatia jamii kugundua manufaa ya kijamii na kiuchumi yataokanayo na ubunifu kwani ubunifu upo kati kati ya mipango mingi ya kiuchumi ya nchi nyingi.

 

Bwana Gurry amesema takwimu hizo ambazo zinazingatia vigezo 80 ni muhimu kwa watunga será na katika kufuatilia masoko na pia utendaji wa nchi katika soko la uchumi. Ripoti pia imetaja nchi zinashika nafasi ya juu ambapo Switzerland inaongoza katika ubunifu ikifuatiwa na Sweden, Marekani, Netherlands na Uingereza ikishika nafasi ya tano.  Ripoti hiyo ya GII imetaja nchi zinazoongoza katika mtazamo wa kikanda kuwa ni India, Afrika Kusini, Chile, Israel na Singapore huku China, Viet Nam na Rwanda zikiibuka kidedea katika makundi ya kiuchumi.

 

Shirika la WIPO limesema vipimo vya GII ni muhimu kwa ajili ya watunga sera kupata uelewa kiasi kuhusu mbinu za kuimarsiha ubunifu kama kiungo muhimu cha maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Ripoti hiyo ambayo imetafiti chumi 129 imezingatia vigezo vikiwemo vya zamani vya utafiti na maendeleo ya uwekezaji na uandikishaji wa hakimiliki na hatimiliki pia ubunifu wa kisasa ikiwemo app za simu na bidhaa za kiteknolojia zinazouzwa nje.

 

WIPO inasema licha ya kupungua kwa ukuaji wa kiuchumi, ubunifu unaendelea kuimarika hususan barani Asia lakini kuna wasiwasi kufuatia misukosuko ya kibiashara na ulinzi. Hatahivyo mipango mizuri ya ubunifu na serikali ni muhimu kwa ajili ya kupata mafanikio.

Bwana Gurry ameongeza kwamba, “nchi ambazo zinatoa kipaumbele kwa ubunifu katika nafasi yao ya ubunifu zinapiga hatua.” Akisema “Kuimarika katika GII kwa nchi kama China na India kumeleta mabadiliko ya ubunifu kikanda na hii ni ishara ya hatua za kisera kwa jaili ya kuimarisha ubunifu.”

Kipimo cha ubunifu duniani 2019 (Isitumike kama picha)
UN News Kiswahili
Kipimo cha ubunifu duniani 2019 (Isitumike kama picha)

 

Ripoti ya mwaka huu wa 2019 ya GII imebeba kauli mbiu “kutengeneza maisha – mustakabali wa ubunifu wa kitabibu”. Huku ripoti ikitambua ubunifu wa kiafya kupitia akili bandia na app za simu ambavyo vyote vitbadili uwasilishaji wa huduma ya afya.