Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ubunifu wa wanawake wabadili jamii zao #WorldIPDay

Katika siku ya kimataifa ya wasichana katika ICT, wasichana hawa wanajifunza programu mbalimbali na uundaji wa roboti, ni miongoni mwa washiriki 150 kwenye warsha na ufuatiliaji wa teknolojia kwenye makao makuu ya ITU, Geneva Uswis.
Picha na (NAMS)

Wanawake

Ubunifu wa wanawake katika nyanja mbalimbali kuanzia mavazi, tiba na hata ufugaji sasa unadhihirisha kuwa udadisi wa kundi hilo ukijengewa uwezo, umaskini utasalia historia.

Katika siku ya haki ya ubunifu duniani, Umoja wa Mataifa unaweka bayana utambuzi wake wa mchango wa wanawake katika udadisi wao na ubunifu wa mbinu mbalimbali za kuleta mabadiliko na maendeleo chanya kwenye jamii zao.

Shirika la hakimiliki duniani, WIPO linasema wanawake wamekuwa mstari wa mbele katika ubunifu kwa lengo la kusaka suluhu ya matatizo yanayokumba dunia hivi sasa na hata siku za usoni.

WIPO imemtolea mfano Filomena Dos Anjos, mwanasayansi wa masuala ya afya ya Wanyama kutoka Msumbiji ambaye ameibuka na mbinu mpya ya kukabili ugonjwa wa kideri miongoni mwa kuku wa kienyeji.

SASA KUKU WA KIENYEJI WANAFUGIKA BILA HOFU YA KIDERI

Bi. Dos Anjos amebuni chanjo dhidi ya kideri inayostahimili joto na hivyo kuweza kuwafikia wafugaji bila kuharibika hata kwenye maeneo ambako si rahisi kuhifadhi chanjo hiyo katika kiwango cha joto kinachotakiwa.

Hata wakati wa majanga, bado kuku hasahauliki kutokana na umuhimu wake kwa jamii husika. Hawa ni wakimbizi wa Sudan Kusini walioamua kuwa moja ya virago vyao ni kuku.
Samuel Okiror/IRIN
Hata wakati wa majanga, bado kuku hasahauliki kutokana na umuhimu wake kwa jamii husika. Hawa ni wakimbizi wa Sudan Kusini walioamua kuwa moja ya virago vyao ni kuku.

Kuku wa kienyeji ni chanjo muhimu cha protini na pia kipato nchini Msumbiji na hivyo kupitia ubunifu wake kuna hakikisho la ustawi wa kiafya na kiuchumi kwa jamii yake.

Dos Anjos ambaye kwa sasa anashirikiana na wanawake na wafugaji vijana kuchagiza matumizi ya chanjo hiyo, ni mshindi wa tuzo ya WIPO ya AWARD yam waka 2018.
WIPO imesema kila uchao hivi sasa wanawake na wasichana wanajiunga na masuala ya Habari, teknolojia, mawasiliano na sayansi na hivyo kuongeza kasi ya mabadiliko chanya katika jamii.

Haki za ubunifu  ni pamoja na hataza, hakimiliki, nembo za biashara na ubunifu viwandani.