Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

‘Arobaini’ ya madalali wa dawa duniani yatimia, WIPO yaingia  ubia na kampuni za dawa

Upatikanaji wa shehena za dawa ni changamoto iwapo madalali wanaweka bei za juu tofauti na zile za kampuni za dawa
WHO
Upatikanaji wa shehena za dawa ni changamoto iwapo madalali wanaweka bei za juu tofauti na zile za kampuni za dawa

‘Arobaini’ ya madalali wa dawa duniani yatimia, WIPO yaingia  ubia na kampuni za dawa

Afya

Shirika la hakimiliki duniani, WIPO limeingia ubia na kampuni za kutengeneza dawa duniani kwa lengo la kuondoa mkanganyiko unaoibuka wakati wa kubaini iwapo dawa za kutibu magonjwa zina haki za hataza au la.

Mkurugenzi Mkuu wa WIPO Francis Gurry ameiambia Idhaa ya Umoja wa Mataifa katika mahojiano maalum huko Geneva, Uswisi kuwa ubia huo unahusisha kuwa na wavuti wenye kanzi data za dawa hizo.

Amesema lengo la ushirikiano na kampuni hizo 20 za kutengeneza dawa duniani ni “kuongeza uwazi kwa kiasi kikubwa katika mchakato huu mzima ili iwe rahisi sana kwa wakala wa manunuzi kuweza kutambua iwapo dawa fulani haina hataza au ina hataza na wapi aende ili kupata taarifa zaidi. Tunachojaribu kufanya hapa ni kuboresha mfumo wa manunuzi."

Mkuu huyo wa WIPO ametoa mfano kuwa "iwapo mashirika ya kiraia yanahusika na ununuzi wa dawa kwa ajili ya matibabu mashinani hayakumbwi na vikwazo katika kutafuta dawa. Nadhani hakuna ambacho sekta ya dawa inafanya hapa zaidi ya kuweka wazi mfumo wa kupata dawa zao kwa urahisi na kuwa wazi juu ya aina ya haki za hataza kuhusu dawa hizo.”
 
Bwana Gurry amesema dawa zitakazowekwa kwenye kanzi data hiyo ni zile zote ambazo ziko kwenye orodha ya shirika la afya ulimwenguni WHO lakin pia watagusia pia mbinu za kitabibu za magonjwa kama vile kisukari, homa ya ini aina ya C ikiwa ni sehemu ya kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs ya kutaka mfumo wa Umoja wa Mataifa kuingia ubia na sekta binafsi na kutumia teknolojia kuboresha afya.