Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Afrika Kusini yachomoza kwenye usajili wa hataza ugenini

Mkurugenzi Mkuu wa WIPO Francis Gurry (kushoto) na Mkuu wa Uchumi Carsten Fink wazungumza na waandishi wa habari katika uzinduzi wa Ripoti ya Viashiria vya Mali ya Ulimwengu. (Picha: WIPO / Berrod).

Afrika Kusini yachomoza kwenye usajili wa hataza ugenini

Afrika Kusini imechomoza katika kuwasilisha maombi ugenini ya kusajili hati ya kisheria ili kuepusha kuigwa na watu wengine au hataza.

Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti mpya ya shirika la hakimiliki la Umoja wa Mataifa, WIPO iliyotolewa leo huko Geneva, Uswisi ikiangazia viashiria vya hakimiliki duniani kwa mwaka 2016.

Mkurugenzi Mkuu wa WIPO Francis Gurry amewaambia waandishi wa habari kuwa usajili wa hataza nje ya nchi unaashiria jinsi wabunifu wanavyotaka kueneza teknolojia nje ya mipaka.

Idadi kubwa ya hataza hizo zilisajiliwa Marekani ambapo Bwana Gurry ametaja nchi zingine za kipato cha kati kuwa ni Brazil, India, Malaysia na Mexico.

Ulimwenguni, nchi zilizoongoza kwa raia wake kusajili hataza ugenini ni Marekani, Japan, Ujerumani na Korea Kusini, huku China ikiongoza kwa kusajili hati zote za hataza, nembo ya biashara na ubunifu wa viwandani.

Hataza zilizoshika kasi zaidi ni teknolojia ambapo Bwana Gurry amesema kunaashiria mwelekeo wa hakimiliki kuwa za kimataifa na ari ya wahusika kupeleka bidhaa zao kwenye masoko ya kigeni.