Kuwait yapokea fidia nyingine ya dola milioni 270-UN

23 Julai 2019

Tume ya fidia ya Umoja wa Mataifa leo imelipa dola zingine milioni 270 kwa serikali ya Kuwait kama sehemu ya fedha za dai la fidia lililobaki la nchi hiyo.

Tume hiyo ya fidia ya Umoja wa Mataifa ilianzishwa mwaka 1991 baada ya vita kati ya Iraq na Kuwait kwa kufuata maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa namba 687 na 692 yote ya mwaka 1991 ili kushughulikia madai na kulipa fidia kwa ajili ya hasara na uharibifu uliotokea kwa watu binafsi, mashirika, serikali na mashirika ya kimataifa.

Na hii ilikuwa ni matokeo ya moja kwa moja ya uvamizi wa serikali ya Iraq na ukaliaji wa Kuwait uliofanyika kati ya a Agosti 1990 hadi 2 Machi 1991.

Tume hiyo ilipokea takribani madai milioni 2.7 na ilikamilisha tathimini ya madai yote mwaka 2005.

Karibu dola bilioni 52.4 zimelipwa kwa zaidi ya mashirika ya kimataifa na serikali 100 ambazo zimegawanywa kwa madai yapatayo milioni 1.5

Uvamizi wa Iraq Kuwait mbali ya kukatili maisha ya watu wengi ulisababisha uharibifu mkubwa wa nyumba, barabara, mitambo na miundombinu mingine muhimu.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter