UN yazindua mradi wa kukwamua ujenzi wa Iraq

Huko Kuwait, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres
UN/Stéphane Dujarric
Huko Kuwait, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres

UN yazindua mradi wa kukwamua ujenzi wa Iraq

Amani na Usalama

Mkutano wa kujadili ujenzi mpya wa Iraq ukifanyika nchini Kuwait, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema licha ya uharibifu mkubwa uliosababishwa na vita nchini humo, bado wairaq wamejitahidi kutoa asilimia 80 ya misaada ya kibiandamu kwa ajili ya wenzao.

Akizungumza kwenye mkutano huo kwenye mji mkuu wa Kuwait, Kuwait City Bwana Guterres amesema wakati wote wa mzozo, wairaq hawakutetereka kwenye tabia yao ya kukirimiana ambapo familia na jamii zilifungua milango kwa waliokuwa wanakimbia madhila.

(Sauti ya Antonio Guterres)

“Mimi mwenyewe nilishuhudia wairaq wasio na chochote kabisa lakini walisaka njia ya kupata rasilimali za kusaidia wengine.”

Bwana Guterres amesema kwa kuwa sasa vita imemalizima kuna kazi kubwa ya kusaidia siyo tu ujenzi bali pia wakimbizi wa ndani na wanaorejea makwao, hivyo amezindua mpango wa Umoja wa Mataifa wa kuikwamua Iraq.

Darasa moja katika jengo la shule lililobomolewa wakati wa vita huko Ninewa Governorate, Iraq
UNICEF/UNI199916/Jemelikova
Darasa moja katika jengo la shule lililobomolewa wakati wa vita huko Ninewa Governorate, Iraq

(Sauti ya Antonio Guterres)

 “Mpango huu wa miaka miwili unalenga kusaidia serikali ya kuchagiza mifumo ya kijamii ya ujenzi mpya. Unalenga kuboresha maisha ya kila siku ya wairaq, badala ya kusubiri mipango ya muda mrefu inayoendana na miradi mkubwa ya miundombinu na marekebisho ya kiuchumi. Utaleta matumaini na fursa.”

Katibu Mkuu amesihi washiriki wa mkutano huo kuchangia mpango huo kisiasa na kifedha.