Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO yapokea msaadawa dola milioni 5 za kuisaidia Yemeni

Sekta ya kilimo imeelezwa kuwa na mchango mkubwa katika kukuza uchumi na kuleta maendeleo kwa mujibu wa ripoti ya FAO. Picha na FAO

FAO yapokea msaadawa dola milioni 5 za kuisaidia Yemeni

Amani na Usalama

Vita vimechangia kwa kiasi kikubwa kutokuwepo na uhakika wa chakula nchini Yemen, kwani wakulima kama raia wengine wamefungasha virago kukimbia machafuko. Sasa mashirika ya Umoja wa Mataifa kama la chakula na kilimo FAO yanafanya juu chini kuwasaidia wakulima kufufua kilimo  na misaada kutoa kwa wahisani inahitajika. Leo Kuwaiti imetoa dola milioni 5 zitakazopiga jeki nia ya FAO yemen.

Shirika la chakula na kilimo duniani, FAO limepokea ufadhili wa dola milioni tano kwa ajili ya kuwasilisha viafaa muhimu vya kilimo nchini Yemen kwa lengo la kuimarisha uhakika wa chakula na lishe wakati nchi hiyo ikikabiliwa na janga kubwa zaidi duniani la chakula.

Ufadhili huo wa mpango wa FAO wa dharura kwa ajili ya Yemen utasaidia watu milioni 8.4 wanaokabiliwa na njaa.

Katika majimbo ya Ibb na Lahij, wakulima watafaidika kupitia ukarabati wa mitaro kwa ajili ya umwagiliaji, kuimarisha mbinu za jadi za kuvuna maji, kuhusisha wanawake na vijana katika uhifadhi wa maji, kazi kwa malipo kwa ajili ya kaya zilizoko hatarini, kuzuia hatari ya mafuriko na kusaidia wakulima kutumia ardhi kwa ajili ya kilimo chenye tija.

Akizungumzia ufadhili huo mwakilishi wa FAO katika ofisi ya Mashariki ya karibu na Afrika Kaskazini, mjini Cairo amesema ufadhili huo wa Kuwait ni muhimu katika kujengea mnepo jamii zilizoko Yemen na kuimarisha ushirikiano wa FAO na Kuwait katika kutatua changamoto za kikanda.

Kwa upande wake mwakilishi wa kudumu wa Kuwait kwenye Umoja wa Mataifa, mjini Geneva amesema, makubaliano hayo yanafungua ukurasa mpya kati ya taifa lake na FAO na kusisitiza umuhimu wa kufanya kazi pamoja ili kuimarisha juhudi za msaada wa kibinadamu kwa ajili ya watu wa Yemen.

Mzozo wa Yemen umeongezeka tangu Machi 2015 na kugharimu kwa kiasi kikubwa Wayemeni ambapo asilimia 75 ya watu nchini humo sawa na watu milioni 22.2 hivi sasa wakihitaji msaada wa kibinadamu.