Fursa ya kuhakikisha SDGs zinatimia ni sasa:ECOSOC

9 Julai 2019

Nchi zote duniani sasa zina fursa ya kipekee ya kuzungumza na kujifunza kutoka kwa wengine amesema leo Inga Rhonda king, Rais wa Baraza la kiuchumi na kijamii la Umoja wa Mataifa ECOSOC katika ufunguzi wa mjadala wa kila mwaka wa ngazi ya juu kuhusu malengo ya maendeleo endelevu (HLPF) ulioanza hapa mjini New york Marekani.

Mkutano wa HLPF ndio mkutano mkubwa unaotathimini mafanikio, changamoto na masuala ya kujifunza katika mchakato wa kuelekea utimizaji wa malengo 17 ya maendeleo endelevu au SDG’s ifikapo mwaka 2030.

Kaulimbiu ya mkutano wa mwaka huu ni “Uwezeshaji wa watu na kuhakikisha ujumuishwaji na usawa” Bi. King amesema “Huu ni wakati wa kimataifa ambako sote tuko hapa, tunahitaji kutumia fursa hii kwa kila hali, zungumzeni ili sote tufaidike na fursa hii.”

Jukwaa hilo litatathimini hatua zilizopigwa katika miaka minne iliyopita tangu malengo hayo yalipopitishwa na nchi wanachama kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa na kuamua nini kinachohitajika kufanyika katika kusongesha mbele ajenda hiyo ya 2030 na wapi tulipofikia kwa pamoja katika utekelezaji wa SDG’s kimataifa, kikanda, kitaifa na mashinani.

Bi. King amesema mkutano huo sio mwisho bali ni jukwaa la kimataifa kudhihirisha uzoefu na kuunda ushirika “sote tunahitaji kujifunza kutoka kwa wenzetu ili tuweze kurejea nyumbani tukiwa tumepata uzoefu mpya wa kutuwezesha ahatimaye kufikia lengo kwa watu wetu, dunia yetu na maratajio yetu.”

Malengo ya SDG’s yanayomulikwa

Malengo yanayomulikwa katika katika mjadala huu ni lengo namba 4 la kuhakikisha elimu jumuishi na bora kwa wote, lengo namba 8 la kuchagiza ukuaji endelevu, jumuishi wa uchumi na ajira zenye hadhi kwa wote, lengo namba 10 lililojikita katika kupungusa pengo la usawa ndani na miongoni mwa nchi, lengo namba 13 la kuchukua hatua haraka kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na athari zake, lengo namba 16 la kuchagiza jamii zenye amani na jumuishi kwa ajili ya maendeleo endelevu , kutoa fursa kwa masuala ya haki kwa wote , uwajibikaji na taasisi imara na jumuishi katika ngazi zote, na lengo la mwishi ni lengo namba 17 ambalo ni la kuimarisha utekelezaji na kufufua ushirika wa kimataifa kwa ajili ya maendeleo endelevu.

Ripoti mpya ya SDG’s

Umoja wa Mataifa pia leo umezindua ripoti yake mpya kuhusu SDGs ambayo imehitimisha kwamba ingawa kuna hatua ambazo zimepigwa “bado kuna changamoto lukuki za kushughulikia”. Ripoti hiyo inasema kuna ushahidi dhahiri wa hatua zilizopigwa katika kupunguza umasikini, masuala ya chanjo na kuongeza fursa za upatikanaji wa nishati kama ya umeme, lakini pia ripoti hiyo imeonya kwamba hatua za kimataifa hazitoshelezi kwani zimewaacha watu wengi wa makundi ya wasiojiweza na nchi masikini wakitaabika zaidi.

Kwa ujumla imeonyesha kwamba mabadiliko ya tabianchi na ongezeko la kutokuwepo usawa sio tu kwamba vinaathiri hatua za kufikia malengo ya mendeleo endelevu ifikapo mwaka 2030 bali pia yanatishia kugeuza mafanikio mengi yaliyopatikana katika muongo uliopita.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter