Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Malengo ya Maendeleo Endelevu yanaweza kufikiwa ‘licha ya nyakati zetu mbaya: Rais wa ECOSOC 

Wanafunzi wakihudhuria tukio baada ya masomo nchini Madagascar.
© UNICEF/Rindra Ramasomanana
Wanafunzi wakihudhuria tukio baada ya masomo nchini Madagascar.

Malengo ya Maendeleo Endelevu yanaweza kufikiwa ‘licha ya nyakati zetu mbaya: Rais wa ECOSOC 

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Licha ya miaka miwili ya "mapambano ya kushangaza" dhidi ya janga la COVID-19, na huku kukiwa na changamoto zinazoongezeka za ulimwengu, matumaini ya kupatikana kwa maendeleo endelevu yanaendelea.” Amesema hii leo Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa la masuala ya Kiuchumi na Kijamii, ECOSOC, Collen Vixen Kelapile. 

Collen V. Kelapile, alikuwa akitoa hotuba ya ufunguzi kwa mawaziri katika Jukwaa la Kisiasa la Ngazi ya Juu la Maendeleo Endelevu (HLPF) linaloendelea katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani. 

Nchi zinakutana katika Ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ili kutathimini jinsi sera za urejeaji katika hali nzuri zinaweza kubadilisha athari mbaya za janga la Covid-19 kwenye lengo moja la kuunda mustakabali wenye usawa zaidi kwa watu wote na sayari. 

Fursa ya mabadiliko 

Bwana Kelapile amewaeleza mawaziri hao kuwa changamoto za sasa za kimataifa lazima zisififishe azimio na uamuzi wao akisisitiza kwamba mataifa lazima yafanye kazi pamoja kwa mshikamano. 

"Baada ya miaka miwili ya mapambano dhidi ya janga hili, ni kweli kwamba sasa tunaishi katika ulimwengu wa kuongezeka kwa migogoro, ukosefu wa usawa, umaskini, na mateso; ukosefu wa utulivu wa kiuchumi; nishati na shida ya chakula inayokuja; kuongezeka kwa viwango vya deni; ya kudorora kwa maendeleo kuelekea usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake.” Amesema na akaongeza kuwa, "na hata hivyo, moja ya ujumbe muhimu ambao tumesikia katika siku chache zilizopita za Jukwaa la Kisiasa la Ngazi ya Juu ni kwamba, licha ya nyakati zetu za huzuni kuna hali ya matumaini kwamba Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu inatupatia mfumo wa kujijenga vizuri zaidi."

Guterres: Janga la chakula na nishati 

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, kwa upande wake amesisitiza haja ya kukabiliana na janga la chakula, nishati na fedha, akisema kwamba uzalishaji wa chakula wa Ukraine, na chakula na mbolea zinazozalishwa na Urusi, lazima zirejeshwe katika masoko ya dunia, licha ya vita inavyoendelea. 

"Tumekuwa tukifanya kazi kwa bidii katika mpango wa kuruhusu usafirishaji salama wa vyakula vilivyozalishwa Ukraine kupitia Bahari Nyeusi na vyakula na mbolea za Kirusi kwenye masoko ya kimataifa. Nashukuru serikali zinazohusika kwa ushirikiano wenu unaoendelea.” Amesema Guterres. 

Ikiwa ni sehemu ya mradi wa 'kijani' wa UNDP, mafundi wakiweka mitambo ya nishati ya jua katika chuo cha polisi mjini Rajaf, Sudan Kusini 21 Agosti 2018
UNDP/Louis Fourmentin
Ikiwa ni sehemu ya mradi wa 'kijani' wa UNDP, mafundi wakiweka mitambo ya nishati ya jua katika chuo cha polisi mjini Rajaf, Sudan Kusini 21 Agosti 2018

Kushughulikia ukosekanaji wa usawa wa kiuchumi 

Hata hivyo, majanga ya leo hayawezi kutatuliwa bila suluhu la janga la kukosekana kwa usawa wa kiuchumi katika ulimwengu unaoendelea, ameongeza Bwana Guterres, akitoa wito wa rasilimali zaidi, "nafasi ya fedha", pamoja na kunyumbulika na kuelewa kwa upande wa taasisi za fedha za kimataifa. 

“Tusisahau kwamba wengi wa watu maskini hawaishi katika nchi maskini zaidi; wanaishi katika Nchi za Kipato cha Kati. Iwapo hawatapokea usaidizi wanaohitaji, matarajio ya maendeleo ya Nchi za Kipato cha Kati zenye madeni mengi yataathiriwa pakubwa.” Ameongeza Bwana Guterres. 

Katibu Mkuu pia ametoa wito wa kuwepo kwa Mpango Mpya wa Kimataifa ili nchi zinazoendelea ziwe na nafasi nzuri ya kujenga mustakabali wao wenyewe, na kuleta mageuzi katika mfumo wa fedha wa kimataifa kuwa ule "unaofanya kazi kwa walio hatarini, na sio tu wenye nguvu." 

Wekeza kwa watu 

Janga la Covid limefichua kukosekana kwa usawa dhahiri, ndani na kati ya nchi na nchi, na kama ilivyo kwa majanga yote, ni walio hatarini zaidi na waliotengwa ambao wameathiriwa zaidi. 

“Ni wakati wa kuupa kipaumbele uwekezaji kwa watu; kujenga mkataba mpya wa kijamii, unaozingatia ulinzi wa kijamii wa wote; na kurekebisha mifumo ya usaidizi wa kijamii iliyoanzishwa baada ya vita ya Pili vya Dunia.” akasema Bwana Guterres. 

'Mapinduzi ya Nishati Mbadala' 

Bwana Guterres, kuhusu nishati mbadala amesisitiza kuhusu hatua kabambe ya tabianchi, akionya kwamba vita ya kuhakikisha joto duniani linaishia nyuzi joto 1.5 juu ya viwango vya kabla ya kuanza kwa viwanda vitashinda au kushindwa katika muongo huu. 

"Kukomesha uraibu wa kimataifa wa nishati ya mafuta kupitia mapinduzi ya nishati mbadala ni kipaumbele namba moja," amesema Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa na kuongeza akisema, "nimekuwa nikiomba kusiwe na mitambo mipya ya makaa ya mawe na hakuna ruzuku tena kwa nishati ya mafuta ya kisukuku kwa sababu ufadhili wa nishati ya mafuta ya kisukuku ni ya udanganyifu, na ufadhili wa nishati mbadala ni sawia." 

Rais wa UNGA 

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Abdulla Shahid, yeye amejikita katika umuhimu wa matumaini na mshikamano, ili dunia iweze kuibuka katika kipindi hiki ikiwa na nguvu zaidi, imara zaidi, na endelevu zaidi. 

"Ili kuvunja mzunguko mbaya wa migogoro lazima tufanye zaidi ya 'kutazama' kuelekea mustakabali endelevu zaidi, lazima tuuweke katika vitendo." amesema Bwan shahid. 

Tujifunze kutoka kwenye janga 

Aidha Bwana Shahid ametoa wito wa kuweka uwekezaji mkubwa katika maeneo kama vile ulinzi wa kijamii, kupunguza umaskini na hatua za tabianchi, pamoja na kuwawezesha vijana kama "mawakala wa mageuzi endelevu." 

Changamoto za kawaida, suluhisho za kawaida 

Bwana Shahid pia ametoa wito wa kujitolea kushughulikia hali ya nchi zilizo hatarini zaidi na kwa maendeleo endelevu ya Afrika, ikiwa ni pamoja na msaada wa kufikia chanjo kwa wote, uhakika wa chakula na upatikanaji wa nishati katika bara zima. 

Ingawa janga hili liliijaribu mipaka ya mshikamano wa kimataifa, "ushirikiano wa kimataifa unatawala na mshikamano wa kimataifa unaendelea", Rais wa Baraza Kuu, akiashiria mipango kama vile utaratibu wa usawa wa chanjo ya COVAX, na mazungumzo juu ya mkataba wa janga la kimataifa. 

"Tumeona nchi na jumuiya zikija pamoja ili kutafuta suluhu za pamoja kwa changamoto zinazofanana. Ni lazima tujenge juu ya hili kwa kila njia.” amesema.