Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maneno matupu bila vitendo hayotimiza SDG’s: Amina Mohammed

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bi Amina Mohamed akihutubia kikao cha ufunguzi cha mkutano wa sehemu ya mawaziri cha jukwaa maalum kuhusu maendeleo endelevu SDGs
UN Photo/Loey Felipe
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bi Amina Mohamed akihutubia kikao cha ufunguzi cha mkutano wa sehemu ya mawaziri cha jukwaa maalum kuhusu maendeleo endelevu SDGs

Maneno matupu bila vitendo hayotimiza SDG’s: Amina Mohammed

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Ni lazima tuepuke mwelekeo legevu kuhusu malengo ya maendeleo endelevu au SDGs, hususan unaojikita katika  maneno matupu  bila vitendo ili tuweze kuleta mabadiliko ya utumizaji wa ajenda ya mwaka 2030.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bi Amina J. Mohamed  hiileo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini  New York Marekani, wakati wa ufunguzi wa jukwaa la ngazi ya juu kuhusu SDG’s leo ikiwa ngazi ya mawaziri. 

Bi Mohammed amesema ni miaka mitatu sasa tangu viongozi wa nchi wanachama kupitisha ajenda ya maendeleo ya mwaka 2030 ambyo ni mwongozo wa kuhakikisha kunakuwa na jamii yenye amani na maendeleo endelevu kwa wote.

Ameongeza kuwa licha ya baadhi ya mafanikio yaliyopatikana katika mchakato wa kutimiza ajenda hiyo lakini bado kuna mapungufu ikiwemo kunendelea kuongezeka kwa umasikini katika baadhi ya sehemu za mijini ambapo inatarajiwa kuwa  watu maskini zaidi duniani wataishi mijiniifikapo mwaka wa 2035.

 

Marie Chatardová,rais wa baraza la kijamii na kiuchumi la Umoja waMataifa akihutubia kikao cha mawaziri cha jukwa maalum kuhusu maendeleo endelevu SDGs.
UN Photo/Loey Felipe
Marie Chatardová,rais wa baraza la kijamii na kiuchumi la Umoja waMataifa akihutubia kikao cha mawaziri cha jukwa maalum kuhusu maendeleo endelevu SDGs.

Pia amesema vijana wengi huenda wakasalia bila ya ajira kuliko watu wa makamo na licha ya mchakato wa watu kupata maji safi, kupunguza vifo vya kina mama na watoto, kupambana na ndoa za utotoni , kupanua wigo wa upatikanaji wa nishati ya umeme, kupunguza pengo la ajira, na kudhibiti uharibifu wa misitu unaendelea kusonga mbele , miundombinu ya kuwezesha hayo bado ni changamoto.

Ameongeza kuwa na kwa mara ya kwanza idadi ya watu wasio na lishe bora imeongezeka kutoka milioni 777 mwaka 2015 hadi milioni 815 mwaka 2016 na kuathiri vikali jukumu letu la kuhakikisha hakuna atakayeachwa nyuma.

Kwa upande wa nishati Bi Mohammed amesema bado watu milioni 250 barani Afrika  hawana nishati safi kwa minajili ya  kupikia.

Amesisitiza licha ya changamoto hizo jukwaa hili ni fursa ya kujibu maswali mawili muhimu, Mosi“Je tuko katika msitari unaotakiwa kufikia malengo hapo 2030? Na pili “nini tunachohitaji kufanya tofauti katika miaka ijayo ili kuzaa matunda mazuri?

Naye Rais wa baraza la kiuchumi na kijamii la Umoja wa mataifa ECOSOC, Marie Chatardova amesema, ingawa kuna maendeleo yanayopigwa hayako katika kasi inayohitajika kuweza kufanikisha maendeleo endelevu ifikapo mwaka wa 2030 na hayalingani katika sehemu zote.