Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanawake kutoka Syria na Jordan 'wavunja miiko' na kuinua vipato vya familia zao

Kikundi cha wanawake kutoka Syria na Jordan kimepatiwa msaada na shirika la kazi duniani, ILO na kuanzisha biashara ya pamoja ya kuuza vitamutamu na vyakula huko Jordan.
ILO Video
Kikundi cha wanawake kutoka Syria na Jordan kimepatiwa msaada na shirika la kazi duniani, ILO na kuanzisha biashara ya pamoja ya kuuza vitamutamu na vyakula huko Jordan.

Wanawake kutoka Syria na Jordan 'wavunja miiko' na kuinua vipato vya familia zao

Wanawake

Nchini Jordan, mradi ulioanzishwa na wanawake 6 kwa ajili ya kutengeneza vitamutamu sasa umekuwa na manufaa makubwa siyo tu kwao pekee bali pia kwa jamii zao na ni kutokana na usaidizi kutoka shirika la kazi duniani , ILO. 

Kikundi hicho kikiwa na jina Azeemat Sabaya, au wanawake waliojizatiti, kilianzishwa miaka 6 iliyopita na wanawake sita, watatu wakitoka Syria na watatu wakitoka Jordan.

Wanawake hao walikuwa na lengo la kusaka fursa ili angalau waweze kupata kipato kusaidia familia zao na ndipo wakawa na duka la kuoka vitu vitamutamu kama vile biskuti na visheti wakitumia mashine za kisasa.

Naima Abdoul ni mmoja wao na yeyé anatoka Jordan na anasema, "tulianza kwa kutengeneza vitamutamu, tukazindua Azeemat Sabaya. Lakini baadaye tukaanza kupata oda za vyakula. Jambo zuri ni kwamba tunatengeneza milo ya kijordan, Kisyria na kipalestina. Tunaandaa chochote kile kinachotakiwa. Bidhaa zetu zimeenea maeneo mbalimbali ya Jordan.”

Wakiwa wamevalia makoti  yao meupe, vilemba kichwani, wanawake hawa wanaonekana kwa umakini zaidi wakiweka vitamutamu hivyo kwenye masinia ya chuma tayari kuoka bidhaa hizo.

Nawal Fahed ambaye yeye ni mkimbizi kutoka Syria akisema kuwa maisha yake yalibadilika baada ya kuwa mkimbizi, lakini aligundua kuwa ni lazima wote wafanye kazi, yeye, mumewe na hata watoto wake.  Anasema alilazimika kutafutia kazi watoto wake ili wakidhi maisha ya familia yao.

Nawal anasema kwamba, "nilisikia kuna mafunzo ya ILO. Nilikwenda na rafiki zangu tukawasilisha maombi na tukakubaliwa. Tulifanya mafunzo na nikajua sasa tutafanya vyema kwenye biashara ya vitamutamu.”

Wanawake hao walipatiwa mafunzo awamu ya pili, ya jinsi ya kuanzisha biashara na kuuza bidhaa na kisha wakaunda kundi lao ambalo limepata mafanikio makubwa hata kuweza kuuza bidhaa zao kwa kampuni kubwa ya kuuza bidhaa tamutamu, na sasa Nawal anasema, "awali ilikuwa vigumu kushawishi waume na watoto zetu kuwa tutafanya kazi  nje  ya nyumbani. Tulianza kuja nao na kufanya nao kazi ili kuwaonyesha kazi iko ngumu  kiasi gani. Na pia tukaanza kuwaajiri. Mume wa rafiki yangu alianza kufanya nasi kazi kusambaza oda wakati wa sikukuu ya Eid. Mume wangu alianza kutusaida kuoka na kupika.”