Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Muafaka wa ILO na UNHCR kuleta afueni ya ajira kwa wakimbizi Jordan

Baba na mwana katika kambi ya wakimbizi ya Zaatari nchini Jordan wakipanda baiskeli zao.
UNICEF/Mariam Al-Hariri
Baba na mwana katika kambi ya wakimbizi ya Zaatari nchini Jordan wakipanda baiskeli zao.

Muafaka wa ILO na UNHCR kuleta afueni ya ajira kwa wakimbizi Jordan

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la kazi duniani ILO na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, wametia saini makubaliano mjini Aman Jordan wiki hii, yenye lengo la kuchagiza zaidi fursa za ajira bora kwa wakimbizi wa Syria na jamii zinazowahifadhi nchini Jordan.

Makubaliano hayo yametokana na muafaka wa kimataifa uliotiwa saini mwaka 2016 na pande mbili hizo, ambao ulijikita katika suluhu za muda mrefu za wakimbizi na watu wengine waliotawanywa na vita na mateso.

Makubaliano haya mapya yanaainisha njia mbazo mashirika hayo mawili yatazitumia kuimarisha ushirikiano na uratibu wa miradi ya pamoja inayohusiana na wakimbizi na jamii zinazowahifadhi kuweza kupata ajira bora nchini Jordan.

Njia hizo zinajumuisha haja ya kuhakikisha ulinzi kwa wakimbizi katika shughuli zote kwa mujibu wa misingi ya kimataifa ya ulinzi na viwango vya ajira.

 

Kundi la wakimbizi wa Syria wakiwa  mstarini tayari kuingia darasani huko Bar Elias nchini Lebanon
UNifeed Video
Kundi la wakimbizi wa Syria wakiwa mstarini tayari kuingia darasani huko Bar Elias nchini Lebanon

ILO na UNHCR tayari wanashirikiana katika masuala ya ajira hususan kwenye kambi za Zaatari na Azraq , lakini pia katika kuratibu shughuli za maisha na ujuzi kwa wakimbizi.

Kitu kingine muhimu katika makubaliano hayo ni kuendelea kufanya kazi na mashirika na taasisi za mashinani ili kutatua changamoto zinazowakabilia wakimbizi na jamii katika soko la ajira.

Ushirika huu ni sehemu na hatua za kimataifa za kukabiliana na changamoto kwa wakimbizi wa Syria, kama ilivyoombwa na serikali ya Jorana hatua ambazo zitawasaidia wote, wakimbizi na jamii zinazowahifadhi.

Shughuli zitakazotekelezwa na mashirika hayo ni pamoja na kupeana taarifa za masuala yanayotajwa na jamii za wakimbizi kuhusu haki ya kufanya kazi, maisha, kuweza kusafiri kwa ajili ya ajira, kushirikiana katika huduma za kuwapa wakimbizi kazi zinazoendana na ujuzi walio nao, na kwa pamoja kupigia chepuo suluhu bunifu kwa ajili ya kufanya soko la ajira kuwa rasmi kwa wakimbizi hao.