Achanganya lugha ajikuta amekuwa fundi bomba badala ya sonara kama alivyokusudia

Wakimbizi wa Syria katika kambi ya Za'atari nchini Jordan.
UNICEF/Christopher Herwig
Wakimbizi wa Syria katika kambi ya Za'atari nchini Jordan.

Achanganya lugha ajikuta amekuwa fundi bomba badala ya sonara kama alivyokusudia

Msaada wa Kibinadamu

Video iliyoandaliwa na shirika la kuhudumia wakimbizi UNHCR, inamuonesha mkimbizi mmoja mwanamke kutoka Syria aliyeko ukimbizi nchini Jordan,  ambaye amejikuta akiwa fundi bomba na hata kufundisha wenzake kazi hiyo huko ukimbizini licha ya kwamba kazi yake alikotoka alikuwa ni sonara? Kulikoni? 

Ninaitwa Safaa Sukarria, ni fundi bomba. Safaa akijitambulisha huku akitabasamu. nchini Syria alikuwa Sonara na alipokimbilia Jordan akataka kujiendeleza,

Alijikuta akiingia katika kazi ya ufundi bomba ukimbizini Jordan baada ya kukosea kuelewa neno la kiarabu ‘sabaka’ ambalo kwao Syria linahusika na uyeyushaji vyuma na vito, huku nchini Jordan likimaanisha ufundi bomba.

“Nilijiandikisha kwenye semina ya utengenezaji wa vito. Lakini kumbe nikakuta ni mafunzo ya ufundi bomba.”

Safaa anaonekana akiwaelekeza wanawake wenzake kukarabati mabomba ya maji na ya vyoo.

Kwa kuanzia, alikuwa anawatengenezea mabomba ndugu na jamaa. Lakini baadaye shughuli ikakua akawafundisha wanawake 25.

Hawa ndiyo wakageuka kuwa kikosi chake cha mafundi wakikarabati mabomba, matanki ya maji na vyoo. Safaa anasema,

“Siyo kazi ya mwanaume au mwanamke. Ni suala la ujuzi. Baadhi ya wanaume wananiambia kwa hivyo wewe ni mwanamke mwenye misuli yenye nguvu, unafikiri wewe ni mwanaume? Ninapata maoni mengi kama hayo lakini ninayapuuza.”

Hii leo Safaa anamiliki biashara nchi nzima ya Jordan na pia kituo pekee katika ukanda huo cha kufundisha wanawake kazi ya ufundi bomba.