Msimu wa baridi, madhila zaidi ya wakimbizi wa Syria nchini Jordan

21 Disemba 2018

Miezi ya msimu wa baridi kali ikinyemelea, ni kumbukizi nyingine ya madhila kwa wakimbizi wa Syria waliosaka hifadhi Jordan ambao wengi wao wanaishi katika mazingira magumu wakati huu ambapo inaelezwa kuwa juhudi za shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR na wadau wake Jordan za kuwapatia vifaa vya kukabiliana na joto zinaonekana kuwa muhimu zaidi.  Taarifa zaidi na Siraj Kalyango.

Mjini Al Mafraq, nchini Jordan kwenye kambi ya wakimbizi kutoka Syria, anaonekana Hilal akiwa amemkumbatia binti  yake. Ni kwenye makazi  yake na mkewe pamoja na watoto wao sita, nyumba ikiwa na vifaa duni vya kuzuia baridi kali, kwenye eneo hili lililoko kaskazini mwa Jordan, anasema, ninafikiri  huu ni msimu wangu wa tano wa baridi nikiwa nje ya Syria, hapa Jordan”

Nyumba yao ikiwa na madirisha na milango yenye nyufa, inaweza kuwa na baridi kali wakati wa baridi lakini hiyo ndiyo pekee wanaweza kumudu.

Hilal na mkewe wanatumia mablanketi na zulia kufunika milango na madirisha akisema kuwa, ‘"wakati wa msimu wa baridi kunapokuwa na baridi, tunawasha kipashajoto tunafunga mlango huu kwa kutumia blanketi na tunafunga dirisha. Tunakiwasha kipashajoto kwa angalau saa moja. Tunapohisi chumba kimepata joto kiasi ninazima. Ninazima kwa saa moja saa moja na nusu nawasha tena. Hivi ndivyo tunavyobana matumizi”

Nihad, mke wa Hilal anasema, anapoogesha watoto, wanahisi baridi kali kwani hata chumba cha bafuni hakina mlango na amepachika kipande cha boksi kuzuia upepo dirishani lakini ukivuma kwa nguvu, boksi hilo huanguka.

Hilal akiwa ana matatizo ya mgongo, maisha yake yanategemea msaada wa fedha anaoupata kutoka UNHCR. Fedha inamsaidia kununua vitu vya kupashia nyumba joto na nguo za msimu wa baridi kwa ajili ya watoto wake.

Hata hivyo anasema kinachoisikitisha zaidi familia hii ni binti yao Milyar mwenye umri wa miaka 11, ambaye anaugua pumu na hivyo msimu wa baridi kali ni shida kubwa.

Hilal anasema alitumia pesa ya kila mwezi kutoka UNHCR kuweka dirisha linalofaa kwenye chumba cha Milyar na kwamba, misaada ya msimu wa baridi inamsaidia sana binti yangu Milyar. Inatusaidia kuweka chumba chenye joto na Zulia, blanket na nguo zas hule ili kumfanya abaki na joto”

UNHCR inasema katika jumla ya dola milioni 180 za kimarekani ilizoomba kwa ajili ya misaada ya msimu wa baridi wa mwaka huu, bado inahitaji dola milioni 32 kusaidia mamilioni ya watu kutoka Syria, Iraq na familia nyingine.

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter