Madhara ya tabianchi ni dhahiri, cha ajabu si watu wote wanatambua- Guterres
Madhara ya tabianchi ni dhahiri, cha ajabu si watu wote wanatambua- Guterres
Dunia inakabiliwa na dharura ya tabianchi, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres wakati akihutubia mkutaon huko Abu Dhabi nchini Saudi Arabia hii leo akisihi washiriki watumie fursa ya sasa kuchukua hatua dhidi ya tabianchi.
Ameonya kuwa madhara yasababishwayo na tabiachi hivi sasa yamezidi na yanampata kila mtu akisema kuwa, “athari ya tabianchi inakwenda kwa kasi kubwa kuliko hata ilivyotabiriwa na wanasayansi.”
Katibu Mkuu amesema madhara ya mabadiliko ya tabianchi “yanazidi juhudi zetu ambapo kila wiki tunashuhudia uharibifu utokanao na mabadiliko hayo kuanzia mafuriko, ukame, mikondojoto hadi vimbunga vikubwa.”
Kwa sababu ya mabadiliko ya tabianchi, “watu duniani kote wanapoteza makazi yao na wanalazimika kuhama. Hali itakuwa mbaya zaidi iwapo hatutachukua hatua sasa tukiwa na matarajio makubwa na dharura kubwa.”
Mabadiliko ya tabianchi yanakwenda kwa kasi kuliko sisi, ni dhahiri hatuna muda wa kupoteza
Wiki iliyopita, ripoti zilisema kuwa theluji kubwa huko Himalaya zinayeyuka kwa kiwango maradufu tangu kuanza kwa karne ya sasa, “ikitishia usambazaji wa maji kwenye maeneo ya Asia ya Kati, Kusini na Mashariki.
Halikadhalika amesema kuwa barafu kuu huko ncha ya kaskazini mwa dunia inayeyuka mapema na inatishia kuachia kiwango kikubwa cha hewa chafuzi aina ya Methane.
“Ni dhahiri kwangu kuwa hatuna muda wa kupoteza,” amesema Katibu Mkuu akisema, “cha kusikitisha kuwa bado si dhahiri kwa viongozi wote watoa maamuzi wanaoongoza duniani”
Ameongeza kuwa kinachotisha zaidi ni kwamba nchi bado haziendi kwa kasi ya kuahidi makubaliano kwenye mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi.
“Kufikia kiwango cha ongezeko la joto duniani katika nyuzijoto 1.5 katika kipimo cha selsiyaji, mwishoni mwa karne ya sasa kunahitaji maamuzi ya haraka na magumu ya juu ya matumizi ya ardhi, nishati, viwanda, majengo, usafiri na miji,” amesisitiza Katibu Mkuu akisisitiza kuwa, “ndio maana naitisha mkutano wa hatua za tabianchi mwezi Septemba mwaka huu.
Abu Dhabi na mwelekeo wa mkutano wa Tabianchi Septemba
Mkutano wa Abu Dhabi ambao ni maandalizi ya mkutano huo wa Septemba wa tabianchi, unaangazia maendeleo yaliyopatikana kwenye maeneo yote ya tabianchi ambayo mkutano huo wa Septemba utasongesha, kuanzia hatua za viwanda, hadi suluhu za kiasili kwa tabianchi sambamba na kuweka kukabili na kuhimili mabadiliko hayo.
Katibu Mkuu amesema mkutano wetu wa Septemba uko wazi, shirikishi na wa dhati na kile tutakachosongesha mbele kinapaswa kuwa fanisi, haki na chenye uwiano kwa wale waliokabiliwa na janga zaidi hivi sasa na pia vizazi vijavyo.
Kwa upande wake, Waziri wa Tabianchi wa Saudi Arabia, Thani Al Zeyoudi, amesema, “tupo hapa leo kwenye ukanda ambao unafahamika kwa uchumi unaotoa hewa chafuzi, lakini kupitia sera za kusonga mbele, sasa tumeweza kufanya nishati ya sola iwe chanzo rahisi zaidi cha nishati.”