Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Septemba viongozi waje na hotuba zenye mashiko na si maneno matupu- Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akiongea na wanahabari (Maktaba)
UN /Mark Garten
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akiongea na wanahabari (Maktaba)

Septemba viongozi waje na hotuba zenye mashiko na si maneno matupu- Guterres

Tabianchi na mazingira

Majira ya joto ya sasa si sawa na majira ya joto ya zama za utoto wangu au enzi za babu zetu! 

Ni sehemu ya hotuba ya Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliyotoa leo kwenye makao makuu ya umoja huo jijini New York, Marekani wakati akizungumza na waandishi wa habari, hotuba ambayo kwa kiasi kikubwa ilijikita kwenye mabadiliko  ya tabianchi na zaidi kiwango cha juu cha joto cha kupitiliza kinachokumba hivi sasa dunia.

Bwana Guterres amesema, “ni katikati ya majira ya joto kwa eneo la kaskazini mwa dunia. Tunashuhudia siyo tu viwango vya juu vya joto vinavyovunja rekodi-bali pia mivutano ya kisiasa nayo inashamiri. Yote  hayo ni hatari na vyote vinaweza kuzuilika.”

Akisisitizia viwango vya juu vya joto, Katibu Mkuu amesema, “tumeishi katika misimu ya joto. Lakini majira haya ya joto si ya zama za ujana wetu. Haya si majira ya joto ya zama za mababu zetu. Kwa mujibu wa takwimu za shirika la hali ya hewa duniani na kituo cha tabianchi, mwezi wa Julai kiwango cha joto angalau kilikuwa sawa ama si kuvuka mwezi ulio na joto zaidi katika historia.”

Viwango vya joto barani Ulaya na baadhi ya maeneo ya kaskazini mwa Afrika ni vya juu na vinatishai afya za binadamu, kilimo na mazingira
WMO Video screen shot
Viwango vya joto barani Ulaya na baadhi ya maeneo ya kaskazini mwa Afrika ni vya juu na vinatishai afya za binadamu, kilimo na mazingira

Katibu Mkuu amesema viwango vya juu vya yote vimevunja rekodi kuanzia New Delhi hadi Anchorage, kutoka Paris hadi Santiago na kutoka Adelaide hadi ncha ya kaskazini mwa dunia. Hivyo  amesema, “iwapo hatuchukui hatua sasa kuhusu tabianchi, hali hizi za hewa za kupindukia ni matukio machache tu kati ya mengi ambayo yatatokea.”

Bwana Guterres akakumbushia mkutano wake alioitisha mwezi ujao wa Septemba jijini New York, Marekani kuhusu tabianchi akisema kuwa, “nimewajulisha viongozi, kuanzia wale wa serikali, biashara na mashirika ya kiraia kuwa tiketi ya kuingilia mkutano huo ni hatua za kijasiri na matarajio makubwa.”

Hatua hizo jasiri kwa mujibu wa Katibu Mkuu zitasaidia kupunguza hewa chafuzi kwa asilimia 45 ifikapo mwaka 2030 na pia kuhakikisha kiwango cha joto hakivuki nyuzi joto 1.5 katika kipimo cha Selsiyasi.

“Tunahitaji kujumuisha athari za mabadiliko  ya tabianchi katika maamuzi yetu yote ili kuwa na ukuaji wenye mnepo, kupunguza hatari na pia kuepusha uwekezaji kwenye vitegauchumi unaoweza kuleta madhara zaidi. Ndio maana nawaeleza viongozi wasije kwenye mkutano na hotuba ‘tamu’ zisizo na uzito,” amesema Katibu Mkuu akiongeza kuwa badala yake, “njooni na mipango thabiti yenye hatua mahsusi kuimarisha michango iliyopangwa ya kitaifa ifikapo mwaka 2020 na mikakati ya kuondokana na hewa ya ukaa mwaka 2050.”

Paneli za sola zitumiazo jua zinatoa nishati safi inayojali mazingira kwa Wazambia wengi (kutoka maktaba)
ILO/Marcel Crozet
Paneli za sola zitumiazo jua zinatoa nishati safi inayojali mazingira kwa Wazambia wengi (kutoka maktaba)

HABARI NJEMA

Hata hivyo Katibu Mkuu amesema tayari kuna habari njema kwa kuwa, “duniani kote serikali, sekta ya biashara na wananchi wanahamasika kukabiliana na janga la tabianchi. Teknolojia iko upande wetu, inatupatia nishati jadidifu katika gharama ya chini zaidi kuliko nishati itokanayo na kisukuku.”

Ametaja pia nishati ya sola na upepo ambavyo ni vyanzo rahisi vya kuzalisha kwa ajili ya kukuza uchumi akitolea mfano bunge la Norway ambalo limepiga kura kuondoa fungu la dola trillioni 1 kutoka mfumo wa nishati  ya kisukuku.

Guterres amesema na mataifa zaidi kuanzia Ethiopia hadi New Zealand, na Fiji hadi Pakistani wanapanda mamilioni ya miti ili kutunza na kuhifadhi misitu na kufyonza hewa ya ukaa.

MIVUTANO YA KISIASA

Kando mwa janga la joto kali linaloambatana na mikondo joto, Katibu Mkuu akaangazia pia mambo mengine matatu yanayosababisha mivutano ya kisiasa hivi sasa duniani.

Mosi ni katika ghuba ya uajemi ambako kuna mvutano juu ya matumizi ya safari za meli na boti kwenye mfereji wa Hormuz na maji yake kwa mujibu wa sheria za kimataifa.

Bwana Guterres amesema kuwa mara kwa mara amekuwa na mazungumzo na viongozi wa pande husika kwa njia ya simu na mikutano na ujumbe mkuu ni kwamba wajizuie kwa kiasi kikubwa kuchukua hatua hasi.

Majira ya joto ya sasa si sawa na majira ya joto ya zama za utoto wangu au enzi za babu zetu! 

Amesema dunia haitaki kushuhudia mvutano mkubwa eneo la ghuba ambao unaweza kuwa na madhara makubwa kwenye usalama na uchumi wa dunia

Jambo la pili ni msuguano wa kiuchumi kati ya mataifa mawili yenye uchumi mkubwa duniani akisema, “tunahitaji kujifunza kutokana na madhara ya vita baridi na tuepushe vita vingine kama hivyo.”

Bila kuzitaja nchi hizo, Katibu Mkuu amesema, “kwa kutazama siku chache zijazo, naona kuna uwezekano wa kuibuka kwa pande mbili za ushindani, kila moja ikiwa na sarafu yake shindanishi, kanuni zake za fedha na biashara, mtandao wake wa intaneti na mfumo wake wa akili bandia pamoja na mtazamo wake wa kijeshi. Bado tuna muda wa kuepusha hili.”

Jambo la tatu ni mvutano kati ya mataifa yenye nguu za kijeshi za nyuklia akisema kuwa mkataba wa matumizi ya kijeshi ya nyuklia ulikuwa ni wa aina yake na ulisaidia kuweka utulivu Ulaya na kukomesha vita baridi.

“Pindi unapomaliza muda wake kesho, dunia itakosa kidhibiti cha vita vya nyuklia. Hii inaweza kuongeza na si kupunguza tishio litokanalo na makombora ya masafa marefu,” amesema Katibu Mkuu.

Kwa mantiki hiyo Bwana Guterres amesihi nchi husika zisake makubaliano ya kudhibiti silaha hizo akisema, “nazisihi kwa dhati Marekani na URusi kupanua wigo wa kile kiitwacho mwanzo mpya wa makubaliano ili uweke utulivu na muda wa kanuni za kudhibiti silaha hizo siku za usoni.”

Halikadhalika ametoa wito kwa nchi wanachama wa mkataba wa kudhibiti matumizi ya silaha za nyuklia, NPT, kushirikiana katika mkutano wa mapitio ya mkataba huo mwaka 2020 ili kuzuia vita vya nyuklia na kutokomeza silaha hizo.

Amekumbusha kuwa ongezeko la mvutano wa kisiasa unakwamisha harakati za kupata suluhu kwenye mizozo kama vile Libya, Syria na Yemen lakini amesema, “tutafanya kila tuwezalo kuimarisha matumizi ya diplomasia kwa ajili ya amani. Katu hatutakata tamaa kwenye juhudi zetu za kusaka amani, kupunguza machungu ya binadamu na kujenga dunia endelevu kwa ajili ya watu na sayari yetu.”