Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Njaa bado ni mtihani mkubwa Afrika na changamoto ni utashi wa kisiasa:FAO 

Mgao wa chakula huko Pieri nchini Sudan Kusini ambako WFP inasaidia watu 29,000 kati yao 6,600 ni watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano. (Picha 5 Februari 2019)
WFP/Gabriela Vivacqua
Mgao wa chakula huko Pieri nchini Sudan Kusini ambako WFP inasaidia watu 29,000 kati yao 6,600 ni watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano. (Picha 5 Februari 2019)

Njaa bado ni mtihani mkubwa Afrika na changamoto ni utashi wa kisiasa:FAO 

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Licha ya kwamba jitihada kubwa zinafanyika barani Afrika kutokomeza njaa tatizo hilo bado limekita mizizi katika maeneo mengi na hatua madhubuti zinapaswa kuchukuliwa haraka ili kuepusha balaa zaidi limesema shirika la chakula na kilimo FAO. Flora Nducha na taarifa zaidi

Kandoni mwa mkutano wa 41 wa shirika la FAO unaoendelea mjini Roma Italia, kikao maalumu kimefanyika kikimulika njaa na lishe barani Afrika, dhumuni likiwa ni kutathimini hatua zilizopigwa katika kutekeleza lengo la kutokomeza njaa na utapiamlo katika bara hilo tangu kupitishwa kwa azimio la Malabo 2014 na malengo ya maendeleo endelevu  au SDG’s mwaka 2015. 

Lakini pia kujadili changamoto zilizopo, matarajio, na kubaini hatua za kuchukua, kubadilishana mawazo na uzoefu katika ngazi ya nchi  na kikanda katika kuhakikisha juhudi zinasonga kuelekea kutokomeza njaa ifikapo 2025.

Akizungumza katika mkutano huo mkurugenzi mkuu wa FAO Jose Graziano da Silva amesema kikubwa ni kukata mizizi ya tatizo hilo amesema, "tunajua kwamba wengi wa watu wanaokabiliwa na njaa hivi sasa ni kutokana na vita na athari za mabadilkiko ya tabianchi , lakini vita vinaundwa na binadamu hivyo tukiwa na utashi wa kisiasa tunaweza kuvikomesha. Na endapo tunaweza será zinazohitajika tutaweza kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.”

Kwa mujibu wa balozi mwema wa FAO kwa ajili ya kutokomeza njaa barani Afrika Dkt. Kanayo Nwanze sera na uwekezaji katika kilimo ni kigingi kikubwa katika utekelezaji wa maazimio kwa kuwa, “ahadi za Malabo haziko katika msitari unaotakiwa, hali ya uhakika wa chakula na lishe bado inaonyesha kuendelea kuzorota Afrika Kusini mwa Jangwa la sahara. Changamoto kubwa tuliyonayo ni katika será za uwekezaji katika kilimo hususan kwa watu wa vijijini.”

Sasa FAO , nchi za Afrika na wadau wengine wa maendeleo wameafikiana kuchukua hatua mujarabu ikiwemo kusaka ufadhili na kuongeza uwekezaji katika kilimo ili kuhakikisha bara la Afrika linarejea katika msitari unaotakiwa kwenye utekelezaji wa azimio la Malabo la kutokomeza njaa ifikapo 2015