Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kilimo cha familia ni nguzo muhimu kufikia SDGs:FAO/IFAD

Vifaa duni vya kilimo kama anavyotumia mama huyu vimekuwa vikiwakwamisha wakulima na kuwafanya wengine kutovutiwa na shughuli hiyo.
FAO/Riccardo Gangale
Vifaa duni vya kilimo kama anavyotumia mama huyu vimekuwa vikiwakwamisha wakulima na kuwafanya wengine kutovutiwa na shughuli hiyo.

Kilimo cha familia ni nguzo muhimu kufikia SDGs:FAO/IFAD

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Shirika la chakula na kilimo FAO na mfuko wa kimataifa kwa ajili ya maendeleo ya kilimo IFAD leo wamezindua muongo wa kilimo cha familia na mkakati wa kimataifa wa hatua za kuzisaidia familia zinazoendesha kilimo hususani katika nchi zinazoendelea.

Mashirika hayo mawili unaongoza utekelezaji wa muongo wa kilimo cha familia uliotangazwa na Umoja wa Mataifa mwishoni mwa mwaka 2017.

Takwimu za mashirika hayo zinasema mashamba ya familia yanawakilisha asilimia 90 ya mashamba yote duniani na asilimia 80 ya uzalishaji wote wa chakula cha dunia.

Hivyo yamesema “Kilimo cha familia ni mdai mkubwa wa kufikia malengo ya maendeleo endelevu SDGs ikiwemo kutokomeza njaa na mifumo yote ya utapiamlo.”

Lengo kuu

Muuongo wa kilimo cha familia lengo lake ni kujenga mazingira bora ambayo yatawezesha kuimarisha uwezo wa wakulima hao na kufikia kiwango cha juu cha mchango wao katika masuala ya uhakika wa chakula na lishe duniani, lakini pia suala la afya, mnepo na mustakabali endelevu.

Mkakati wa hakua wa kimataifa unatoa muongozo kwa jumuiya ya kimataifa kuhusu hatua za pamoja ambazo zinaweza kuchukuliwa kati ya mwaka 2019- 2028.

Pia unaainisha haja ya kuongeza miongoni mwa mambo mengine fursa ya wakulima wa familia katika masuala ya hifadhi ya jamii , mikopo, masoko, mafunzo na fursa za kuzalisha kipato.

Akihimoza hilo katika uzinduzi wa muongo huo mjini Roma Italia mkurugenzi mkuu wa FAO Jose Graziano da Silva amesema “Sio tu kwamba tuna tatizo la njaa ambalo linaongezeka bali pia tuna tatizo la utipwatipwa. Tunahitaji kutilia mkazo utipwatipwa, tunajua nini tunatakiwa kufanya kukabiliana na njaa lakini hatufahamu sana kuhusu kukabiliana na utipwatipwa. Wakulima wa ngazi ya familia ndio wanaozalisha bidhaa katika jamii, zilizo bora na kuzalisha chakula katika njia endelevu, huu ndio mchango wao.”

Naye Rais wa IFAD Gilbert F. Houngbo ameongeza kuwa “Ili kufikia lengo la kutokomeza njaa na umasikini ni lazima tuwekeze katika wakulima wadogowadogo wa ngazi ya familia na kuwasaidia kutumia rasilimali zao, ujuzi, nishati na kuwawezesha ili kubadili maisha yao na ya jamii zao. Chaguo tunalolifanya sasa ndilo litaamua endapo mustakabali wetu wa mfumo wa chakula utakuwa wenye afya, lishe, jumuishi, wenye mnepo na endelevu.”

Na katika barua iliyosomwa kwenye uzinduzi huo Papa mtakatifu Frabcis amesema “Ajira ya vijana katika kilimo , mbali ya kupambana na tatizo la ajira , inaweza kuleta nguvu mpya kwenye sekta ambayo inadhihirisha kuwa na umuhimu mkubwa kwa maslahi ya nchi nyingi. Lengo la ajenda ya 2030 haliwezi kupuuza mchango wa vijana na uwezo wao katika ubunifu.”

Umuhimu wa kilimo cha familia katika SDGs

Kilimo cha familia ndio uti wa mgongo wa wa uzalishaji wa chakula chote duniani, iwe ni kwa mimea, nyama, samaki, bidhaa za wanayama wengine kama mayai au maziwa, na chakula kinacholimwa kama mazao, matunda ya misituni, milimani au katika mashamba ya samaki, vyote hivyo vinadhibitiwa na kuendeshwa na familia na vinategemea sana nguvu ya wanafamilia , wawe wanawake au wanaume.

Pia kilimo cha familia kinahakikisha mafanikio ya kupitisha ujuzi kutoka kizazi kimoja hadi kingine na kuchagiza usawa na faida ya jamii.

TAGS: FAO, IFAD, Kilimo cha familia, njaa, umasikini, chakula, SDGs