Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO yazindua kituo cha tabianchi na maendeleo endelevu kwa Afrika

Wakulima wanachama wa kikundi cha kupanda mboga cha Selam nchini Ethiopia wakiwa kwenye bustani  yao ambapo vijana wengi hivi sasa ambao wako kwenye mtego wa kutumbukia kwenye uhamiaji wamejiweka pamoja na kushiriki kwenye kilimo cha mboga na  matunda
©FAO/Tamiru Legesse

Tabianchi na mazingira

Hatua za kipekee za kuchagiza na kuendeleza maeneo ya vijijini barani Afrika zinahitajika ili kuhakikisha mustakabali bora wa vijana wa bara hilo ambao pindi wanapopatiwa fursa wanaweza kuwa vichocheo vya maendeleo.

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la chakula na kilimo duniani, FAO José Graziano da Silva amesema hayo leo huko Roma, Italia wakait wa uzinduzi wa kituo cha tabianchi na maendeleo endelevu barani Afrika.

Kituo hicho kitasaidia usambazaji na ubadilishanaji wa taarifa kuhusu maendeleo endelevu na suluhu bunifu kwa lengo la kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs na mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabiachi.

Bwana da Silva amesema haiwezekani kuifanya sekta ya kilimo iwe ya kisasa barani Afrika bila kuchochea vijana ambao wengi wao hivi sasa fikra zao ni uhamiaji akisema kuwa , “ tunahitaji vijana vijiijni, tunahitaji maendeleo ya vijijini, na hatuwezi kuwa na mambo hayo mawili bila kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.”

Mratibu wa kikanda wa FAO anaehusika na ofisi ya eneo la Kati mwa Afrika  akitembelea mradi wa  shamba la mboga za majani.
©FAO/Gesrhill Mengome
Mratibu wa kikanda wa FAO anaehusika na ofisi ya eneo la Kati mwa Afrika akitembelea mradi wa shamba la mboga za majani.

Amesisitiza kuwa viwango vya njaa vinazidi kuongezeka katika baadhi ya maeneo barani Afrika na iwapo “hatutachukua hatua sahihi kwenye ukanda wa Sahel, hatutaweza kufanikisha SDGs na kutokomeza njaa mwaka 2030.”

Ni kwa mantiki hiyo kituo hicho ambacho kimeanzishwa ushirikiano baina ya serikali ya Italia, FAO na shirika la mpango wa maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP, kimebainisha mipango ya mawasiliano na usaidizi ikiunganishwa na fursa za kupata fedha na kubaini na kutathmini miradi kwa lengo la kuchagiza, maendeleo endelevu, kilimo kinachojali mazingira, upatikanaji wa maji, nishati salama na usawa wa kijinsia.

Akizungumza kwenye tukio hilo, Msimamizi Mkuu wa UNDP Achim Steiner amesema leo hii, “eneo la Afrika lililo kusini mwa jangwa la Sahara lina viwango vya juu vya ukosefu wa lishe, mazao ya shambani yakiwa ni madogo kuliko kwingineko. Kuna sababu lukuki ikiwemo miundombinu isiyotosheleza, ukosefu wa masoko na mikopo.”