Cameroon tambueni wapinzani kama wadau wa mchakato wa amani- Bachelet

24 Juni 2019

 

Baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa limeanza mkutano wake wa kawaida wa 41 huko Geneva Uswisi hii leo ambapo Kamishna Mkuu wa haki za binadamu Michelle Bachelet amezungumzia masuala ya  ukiukwaji wa haki za binadamu katika maeneo mbalimbali duniani ikiwemo Sudan, Syria na Cameroon.

Bi. Bachelet alianza na Syria ambako amesema makombora yanayoporomoshwa na serikali na wadau wake sambamba na vikundi vilivyojihami yamesababisha vifo vya mamia ya raia, yameharibu miundombinu ya kijamii na kusababisha watu 200,000 kukimbia makazi yao.

Cameroon nako, Bi. Bachelet ameonesha wasiwasi wake juu ya kuendelea kubinywa kwa demokrasia akitolea mfano wa tukio la tarehe mosi mwezi huu ambapo watu 350 walikamatwa kwa kushiriki maandamano yaliyoandaliwa na upinzani.

“Natoa wito kwa mamlaka kuzingatia haki ya uhuru wa kukusanyika. Nasihi pia mamlaka zitazame vyama upinzani kama wadau kwenye mchakato mzima wa mazungumzo ambayo ni muhimu katika kuweka msingi wa amani endelevu nchini Cameroon,” amesema Bi. Bachelet.

Kuhusu Sudan, amestaajabu vile ambavyo maandamano ya amani yaliyokuwa na wito wa kusaka demokrasia nchini humo yamekumbwa na kigingi kutoka serikalini huku vikosi vya usalama vikiripotiwa kufanya msako na kusababisha vifo vya waandamanaji zaidi ya 100, na mamia wengine wamejeruhiwa.

UN Photo/Jean-Marc Ferré
Ukumbi wa Baraza la Haki za binadamu la Umoja wa Mataifa ambamo kwalo wataalamu wa haki za binadamu huchangia hoja kuhusu haki za binadamu

“Nasihi Sudan iipatie ruhusa ofisi yake, ikomeshe ukandamizaji wa haki za binadamu na irejeshe huduma ya intaneti. Wananchi wa Sudan wana haki ya kueleza maoni yao na kama walivyo watu wengine kwingineko, wana haki ya kuishi kwa uhuru na amani, wakifurahia utawala wa sheria na mazingira ya hali ya juu ya kiutu.”

Kamishna Mkuu huyo wa haki za binadamu amezungumzia pia adhabu ya kifo akiitaja Iran ambayo amesema imeendelea kutoa adhabu hiyo kwa watoto.

“Nilichukizwa na hatua ya mamlaka za Ian kuhudumu na kunyonga wavulana wawili wenye umri wa miaka 18 tarehe 1 mwezi Aprili mwaka huu. Nasalia na wasiwasi juu ya idadi kubwa ya watoto wanaosubiri kunyongwa, idadi yao ikikadiriwa kuwa 85,” amesema Bi. Bachelet.

Hata hivyo amepongeza maendeleo yaliyofikiwa katika kutokomeza adhabu ya kifo duniani kwa kuzingatia kuwa mwaka huu ni miaka 30 tangu kupitishwa kwa itifaki ya pili ya mkataba wa kimataifa wa haki za kiraia na kisiasa, ambayo inalenga kutokomeza adhabu hiyo.

Maendeleo hayo chanya ni pamoja na hatua ya hivi karibuni ya Gambia, na Palestina kuridhia itifaki hiyo, huku huko Benin na Burkina Faso kipengele cha adhabu ya kifo kimeondolewa kwenye kanuni ya makosa ya jidani ilhali huko Malaysia na Jimbo la California nchini Marekani adhabu hiyo imesitishwa kwa muda.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud