Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ni wakati wa kurejesha utawala wa raia Sudan: Bachelet

Waandamanaji wakikusanyika mbele ya Makao Makuu ya jeshi la Sudan mjini Khartoum (11 April 2019)
Masarib/Ahmed Bahhar
Waandamanaji wakikusanyika mbele ya Makao Makuu ya jeshi la Sudan mjini Khartoum (11 April 2019)

Ni wakati wa kurejesha utawala wa raia Sudan: Bachelet

Haki za binadamu

Kamishina mkuu wa Umoja wa Mataifa wa haki za binadamu Michelle Bachelet, leo ametoa wito kwa uongozi wa kijeshi nchini Sudan kuachia ngazi baada ya mapinduzi ya wiki iliyopita nchini humo yaliyofanya jeshi kutwaa mamlaka. 

Akizungumza na waandishi wa Habari mjini Geneva wakati wa kuanza kwa kikao cha Baraza la Haki za binadamu kujadili Sudan Bi. Bachelet amesema "Ninawaomba viongozi wa kijeshi wa Sudan na wale wanaowaunga mkono kuondoka madarakani ili kuruhusu nchi hiyo kuanza upya njia ya mageuzi ya kitaasisi na kisheria.” 

Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, "maendeleo muhimu" yamepatikana katika uanzishwaji wa tume ya kitaifa ya haki za binadamu, kuhusu haki ya mpito, ardhi, wanawake na usawa wa kijinsia, mageuzi ya kisheria na mapambano dhidi ya rushwa. 

Kwa Umoja wa Mataifa, jeshi sasa linawajibika kwa ukiukaji kadhaa wa sheria za kimataifa na mapinduzi yaliyofanywa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhane yanakiuka haki za binadamu, katiba na mikataba mingine ya muda iliyoidhinishwa baada ya mapinduzi ya kidemokrasia ya 2019. 

Chini ya masharti haya, Bi. Bachelet, ameelezea utwaaji wa madaraka wa kijeshi wa Oktoba 25 kuwa "unatia wasiwasi sana" na akataka kukomeshwa kwa matumizi ya nguvu kupita kiasi yanayofanywa na wanajeshi na vikosi vingine vya usalama au idara za kijasusi. "Matumizi ya nguvu kupita kiasi kama vile kurusha risasi za moto kukandamiza utekelezaji wa haki hizi ni kinyume cha sheria na haifai," amesema Bi. Bachelet. 
Watu 13 wamefariki na mamia kadhaa kujeruhiwa tangu Oktoba 25 

Tangu Oktoba 25, takriban watu 13 wameuawa na mamia kadhaa kujeruhiwa, kulingana na vyanzo vya hospitali. "Waliohusika lazima wachukuliwe hatua," amesisitiza Bi. Bachelet. 

Kwa mujibu wake, mapinduzi haya yanasaliti mapinduzi ya kijasiri na yenye msukumo ya mwaka 2019 na yanakiuka sheria za kimataifa za haki za binadamu, pamoja na hati ya kikatiba ya nchi na hati zingine za msingi za mpito. 

Michelle Bachelet, Kamishna Mkuu wa haki za binadamu.
UN Photo - Jean-Marc Ferre
Michelle Bachelet, Kamishna Mkuu wa haki za binadamu.

 

Kamishna Mkuu huyo wa haki za binadamu anaamini kwamba matukio ya tangu mapinduzi yamekumbusha ukurasa mbaya katika historia ya nchi hiyo, ambapo uhuru wa kujieleza umeminywa na haki za binadamu zimekandamizwa kabisa. 

Watu wengi wakiwemo mawaziri wa serikali, wanachama wa vyama vya siasa, wanasheria, wanaharakati wa mashirika ya kiraia, waandishi wa habari, watetezi wa haki za binadamu na viongozi wa maandamano wamekamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi kizuizini. 

Kufuatia kuzuiliwa kwake, waziri mkuu aliwekwa chini ya kizuizi cha nyumbani, wakati jana televisheni ya serikali ilipotangaza kuwa mawaziri wanne wataachiliwa.

Kwa Umoja wa Mataifa, njia pekee ya kutoka sasa kwenye mtighani huu ni kujiengua kwa wahusika wamapinduzi. "Ninawaomba viongozi wa kijeshi wa Sudan na wale wanaowaunga mkono kujiondoa ili kuruhusu nchi hiyo kuanza upya njia ya mageuzi ya kitaasisi na kisheria," Bachelet ameliambia Baraza. 
Matarajio ya demokrasia ya watu wa Sudan  

Kulingana na Kamishna Mkuu, watu wa Sudan wana haki ya uhuru wa kujieleza na kukusanyika kwa amani. 
"Lazima tuunge mkono matamanio ya wazi ya watu wa Sudan ya demokrasia na jamii isiyotegemea nguvu za kibabe kiholela, lakini kwa utawala wa sheria matakwa wanayoendelea kuelezea na haki ambayo wanaendelea kudai , kwa ujasiri na heshima kubwa, ni mahitaji ya haki ”, amesihi nchi wanachama wa Baraza. 

Kwa upande wake, Kamati ya Uratibu ya Taratibu Maalum za Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa ilisema "ina wasiwasi mkubwa juu ya athari za hatua zilizotekelezwa tarehe 25 Oktoba na jeshi la Sudan wakati wa kipindi cha mpito ambapo utawala wa kiraia ungeimarishwa nchini Sudan, na pia kwenye makubaliano ya amani ya Juba ”. 

Kulingana na Mwenyekiti wa kamati hii, Victor Madrigal-Borloz, athari kwa demokrasia, utawala wa sheria na kuheshimu haki za binadamu nchini Sudan ziko wazi. 

"Ninaomba Baraza kuchukua hatua zote ndani ya uwezo wake ili kusaidia kufufua mchakato wa amani, ikiwa ni pamoja na hatua za kusaidia kurejesha mara moja na bila masharti ya utawala wa kiraia," amesema Madrigal-Borloz. 

Waandamanaji wameingia mitaani katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum tarehe 11 Aprili 2019,
UN Sudan/Ayman Suliman
Waandamanaji wameingia mitaani katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum tarehe 11 Aprili 2019,

Umuhimu wa kikao cha leo 

Kikao hiki maalum ni cha kuzingatia rasimu ya azimio lililowasilishwa na Uingereza, Ujerumani, Marekani na Norway kutaka utawa wa kiraia kurudishwa mara moja. 

Nchi wanachama wa baraza la Umoja wa Mataifa pia lazima zifikirie Ijumaa rasimu ya azimio linalomtaka Bi Bachelet kumteua "bila kuchelewa" mtaalamu wa haki za binadamu nchini Sudan. 

Mtaalamu huyu atakayeteuliwa anatarajiwa kuwasilisha kwa Baraza la Haki za Kibinadamu katika kikao chake cha 50 ripoti iliyoandikwa inayoangazia hali ya haki za binadamu tangu jeshi kunyakuwa mamlaka, pamoja na ukiukaji na ukiukwaji  wa haki zq binadamu uliofanywa katika kipindi hiki.  

Kwa mujibu wa rasimu ya azimio hilo, mamlaka ya mtaalam atakayeteuliwa kuhusu Sudan yatakoma baada ya kuanzishwa upya kwa serikali ya kiraia. 

Kumbuka kwamba mwaka mmoja uliopita, Baraza la Haki za Kibinadamu liliamua kusitisha mamlaka ya mtaalam huru wa Sudan, baada ya miaka mingi.  
Hali hii iliwezeshwa na mapinduzi ya kidemokrasia ya miaka miwili iliyopita ambayo yalisababisha serikali ya muda ya kiraia nakuirejesha Khartoum ambayo ni mji mkuu na miji mingine kadhaa ya Magharibi katyika utulivu.