UN yalaani mauaji na kushikiliwa kwa waandamanji wakati wa maandamano ya amani Sudan

3 Juni 2019

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, amelaani vikali ukatili na ripoti za matumizi ya nguvu kupita kiasi dhidi ya raia nchini Sudan, vitendo ambavyo vimeripotiwa kusababisha vifo na majeruhi.

Akizungumza na waandishi wa habari hii leo mjini New York, Marekani, msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric amemnukuu Bwana Guterres akilaani matumizi ya nguvu kupita kiasi wakati wa kutawanya waandamanaji kutoka maeneo waliokusanyika na kwamba anatiwa hofu na ripoti za kushambuliwa kwa vituo vya afya.

Katibu Mkuu amekumbusha baraza la mapinduzi la kijeshi nchini Sudan kuhusu wajibu wao kulinda usalama wa raia wa Sudan na kutoa wito kwa pande husika kujizuia ikiwemo kuhakikisha haki za binadamu kwa kila raia ikiwemo uhuru wa kukusanyika na kujieleza.

Aidha Bwana Guterres ametoa wito wa kuhakikisha uwasilishaji salama wa vifaa tiba katika maeneo ya maandamano na hospitali ambako majeruhi wanapokea tiba.

Bwana Guterres amehimiza mamlaka nchini Sudan kuwezesha uchunguzi huru wa vifo na kuwajibisha wahusika.

Ametoa wito kwa pande husika kusaka majadiliano kwa njia ya amani na kuzingatia muongozo kwa ajili ya kukabidhi mamlaka kwa mamlaka inayoongozwa na raia kama ilivyopendekezwa na muungano wa Afrika.

Katibu Mkuu huyo amekumbusha dhamira ya Umoja wa Mataifa kushrikiana na Muungano wa Afrika kwa ajili ya kusaidia mchakato huo na kuelezea utayari wake kusaidia washikadau wa Sudan katika juhudi zao za amani ya kudumu.

Wakati huo huo, Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet amelaani vikali matumizi ya risasi za moto katika maeneo ya waandamanaji mjini Khartoum, ambako kwa mujibu wa duru za habari yamesababisha baadhi ya watu kufariki na wengine kujeruhiwa huku viongozi wao wakizuiliwa.

Taarifa ya Bi. Bachelet iliyotolewa na ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR, imemnukuu akisema, “waandamanaji Sudan kwa kipindi cha miezi michache iliyopita wamekuwa ni mfano mzuri wa maandamano ya amani na kufanya kazi kwa kushirikiana na baraza la mapinduzi la kijeshi.”

Kamishna Mkuu huyo amekwenda mbali zaidi na kusema, “ninalaani kabisa matumizi ya nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanji. Ripoti za matumizi ya risasi za moto kandoni mwa na hata ndani ya vituo vya afya vinasikitisha. Ninatoa wito kwa vikosi vya usalama kusitisha mara moja mashambulizi kama hayo na kuhakikisha ufikiaji wa huduma ya afya na wote.”

Kamishna Mkuu huyo amesistiza kwamba wale ambao wanatekeleza uhuru wao wa kukusanyika kwa amani na kujieleza ni lazima walindwe na sio kulengwa au kuzuiliwa kwani ni msingi muhimu wa haki za binadamu kimataifa.

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter