Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miaka miwili ya vita Ukraine watoto wameishi kwenye mahandakki, suluhu ya kukomesha vita inahitajika: UN

Familia ikipatiwa huduma ya matibabu Odesa baada kukimbilia Kherson Ukraine
© UNICEF
Familia ikipatiwa huduma ya matibabu Odesa baada kukimbilia Kherson Ukraine

Miaka miwili ya vita Ukraine watoto wameishi kwenye mahandakki, suluhu ya kukomesha vita inahitajika: UN

Amani na Usalama

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF limesema robo tatu ya watoto na vijana wenye umri wa miaka 14 hadi 34 nchini Ukraine wameripotiwa hivi karibuni kuhitaji msaada wa kihisia au kisaikolojia.

Katika taarifa yake iliyotolewa leo mjini Kyiv Ukraine shirika hilo limesema “Watoto katika miji Kwenye maeneo ya mstari wa mbele nchini  humo wamelazimika kutumia kati ya saa 3,000 na 5,000 sawa na kati ya miezi minne na karibu miezi 7 kujikinga na vita katika mahandaki ya chini ya ardhi na vituo vya chini ya ardhi vya treni au metro katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, huku mashambulizi anga zikisikika juu ya mahandaki hayo”.

Kwa mujibu wa UNICEF tangu uvamizi kamili wa vita hiyo Februari 2022, mashambulizi yasiyokoma yaliyosababisha karibu arifa 3,500 za uvamizi wa anga katika mikoa ya Zaporizhzhia na Kharkiv na karibu 6,200 katika eneo la Donetsk - yamekuwa na athari mbaya kwa afya ya akili ya watoto na uwezo wa kujifunza kwa ufanisi.

Athari za kisaikolojia

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Catherine Russell amesema "Vita ya Ukraine imesambaratisha maisha ya utotoni na kuharibu afya ya akili ya watoto na uwezo wao wa kujifunza. Watoto wamepitia miaka miwili ya unyanyasaji, kutengwa, kutenganishwa na familia, kupoteza wapendwa wao, kuhamishwa na kuvuruga shule na huduma za afya. Wanahitaji jinamizi hili kukomeshwa.”

Ameongeza kuwa athari za kisaikolojia za vita kati ya watoto zimeenea. Kulingana na takwimu za uchunguzi, nusu ya watoto wenye umri wa miaka 13 hadi 15 wana shida ya kulala, na mtoto 1 kati ya 5 wana msongo wa akili na kupatwa na majinamizi ya yaliyowasibu ikiwa ni hali ya kawaida ya maradhi baada ya kupitia kiwewe. 

Vita imekuwa zahma kubwa kwa watoto na familia zao
© UNICEF
Vita imekuwa zahma kubwa kwa watoto na familia zao

Jumuiya ya kimataifa iongeze juhudi kumaliza vita Ukraine

Wakati huohuo leo wataalm huru wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuongeza juhudi zaidi kukomesha vita inayoendelezwa na Urusi dhidi ya Ukraine kwa kuzingatia katiba ya umoja wa Mataifa na kusaka suluhu kwa njia ya amani bila kuchelewa.

Katika taarifa yao iliyotolewa mjini Geneva Uswis kuadhimisha miaka miwili ya uvamizi kamili wa Urusio nchini Ukraine wataalam hao wamesema “Maisha ya mamilioni ya raia yanaendelea kuwa hatarini kadri vita hiyo inavyoendelea.”

Wameongeza kuwa wato hao ambao ni watoto, wanawake na wanaume ni lazima kila wakati wandewe ubinadamu na kuheshimu utu wao.

Wataalm hao wamesisitiza kuwa, “Kwa watu hao amani si maneno matupu wala dhana ya nadharia. Ni sharti muhimu la kurejesha hali ya kawaida kwa maisha ya kila siku.”

Hivyo wamesema ni muhimu sasa kuliko wakati mwingine wowote kwa jumuiya ya kimataifa kuhakikisha vita nchini Ukraine inakoma.

Msaada muhimu ukiwasili  kwa watu walioathirika na vita Kakhovka Dam blast mashariki mwa Ukraine
© UNICEF Ukraine
Msaada muhimu ukiwasili kwa watu walioathirika na vita Kakhovka Dam blast mashariki mwa Ukraine

Mgogoro mkubwa zaidi barani Ulaya: WHO

Nalo Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Ulimwenguni WHO limeitaja hali ya Ukraine kuwa ni dharura kubwa zaidi barani Ulaya.

WHO imekuwa ikishirikiana na wizara ya afya nchini humo ili kubaini, kwa wakati muafaka, mahitaji muhimu ya sekta hiyo ni yapi na kuchukua hatua inapohitajika ili kuimarisha mifumo iliyopo ya afya.

WHO inasema “msaada umejumuisha kuchangia mara kwa mara vifaa muhimu vya matibabu, magari ya kubeba wagonjwa na vifaa ili kuhakikisha vituo vya afya vilivyopo vinaweza kuendelea kufanya kazi.”

Pia WHO imejenga miundo mbinu ya muda katika jamii ambapo vituo vya afya vimeharibiwa au kusambaratishwa na hivyo kuhakikisha kwamba watu wanaweza kuendelea kupata huduma. 

Hivi sasa, kliniki 12 za kawaida za huduma za msingi ziko wazi katika maeneo kote kusini na mashariki mwa nchi.

WHO imethibitisha jumla ya mashambulizi 1,574 dhidi ya vituo vya afya tangu vita vilipozuka, na kugharimu maisha ya wahudumu 118 wa afya, na kuathiri vituo vya afya, usafiri na maghala.

Msaada ukitolewa katika kituo cha kiraia kwa wakazi wa  Bakhmut karibu na msitari wa mbele wa vita Ukraine
© UNOCHA/Oleksandr Ratushniak
Msaada ukitolewa katika kituo cha kiraia kwa wakazi wa Bakhmut karibu na msitari wa mbele wa vita Ukraine

OCHA yalaani mashambulizi mapya

Mratibu wa Misaada ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Ukraine, Denise Brown, amelaani vikali mashambulizi mapya leo katika miji ya Odesa na Dnipro. 

Mamlaka za mitaa zimeripoti kuhusu vifo vya raia kadhaa, pamoja na uharibifu wa nyumba.

Mashambulizi haya katikati na kusini mwa Ukraine yanakuja siku moja tu baada ya mashambulizi mabaya katika mkoa wa Donetsk, mashariki mwa nchi. 

Mamlaka ya Ukraine inasema hifadhi ya nafaka na miundombinu ya kiraia ikiwa ni pamoja na kiwanda cha kuzalisha umeme zimeathirika.

Bi. Brown amesema “mashambulizi haya ya hivi karibuni kwa mara nyingine tena yanatukumbusha madhara yasiyofikirika ambayo vita vya Shirikisho la Urusi vimewapata watu wa Ukraine huku vifo, hasara na uharibifu vikiwa ni hali halisi ya kila siku kwa mamilioni ya watu wanaoishi katika jamii zilizo mstari wa mbele.

Hata hivyo OCHA inasema mashirika ya kibinadamu yanaendelea kufanya kila e yawezavyo kusaidia watu walioathiriwa na mashambulizi haya yanayoendelea.

Katika mji wa Odesa na Dnipro leo, OCHA ilijiandaa kutoa huduma ya kwanza na usaidizi muhimu, kusambaza vinywaji na chakula cha moto, pamoja na vifaa vya ukarabati. 

Umoja wa Mataifa na washirika pia wanatoa msaada wa kisaikolojia na ushauri wa kisheria kwa wakazi ambao nyumba zao zimeharibiwa.