Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto zaidi ya milioni 1.3 wapata chanjo Msumbiji:UNICEF

Mtoto akichanjwa
PATH
Mtoto akichanjwa

Watoto zaidi ya milioni 1.3 wapata chanjo Msumbiji:UNICEF

Afya

Watoto 700,000 wamepatiwa chanjo ya polio nchini Msumbiji huku wengine 650,000 wakichanjwa dhidi ya surua na rubella, imesema taarifa iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF.

Taarifa hiyo inasema mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini Msumbiji zimesababisha madimbwi mengi na visima kufurika hususan katika maeneo ya vijijini na sasa mashirika ya kimataifa ya misaada ya kibinadamu yanatoa msaada wa maji safi na salama kwa maefu ya familia zilizotawanywa.

UNICEF imesema maelfu kwa maelfu ya watoto walioathirika na kimbunga Idai nchini Msumbiji walichanjwa wiki iliyopita na kupewa matone ya vitamini. Kwa ushirikiano na wadau wengine kama shirika la afya duniani WHO, shirika la UNICEF lilisaidia hatua za wiki ya dharura iliyoongozwa na serikali ya Msumbiji katika wilaya 21 kwenye majimbo ya Sofala, Manica, Inhambane na Zambezia.

Chanjo kwa Watoto

Kwa mujibu wa UNICEF watoto zaidi ya laki 7 wamepatiwa chanjo ya polio na wengine zaidi ya 650,000 wamechanjwa dhidi ya magonjwa ya surua na rubella.

Wahudumu wa afya pia wamefanikiwa kuwafikia watoto laki 7 na kuwapa matone ya vitamini A, kuwapa dawa ya minyoo watoto 550,000 na barubaru zaidi ya 650,000 dawa na madini ya chuma na Folic Acid.

UNICEF inasema inashukuru “kwa juhudi kubwa zilizofanywa na timu ya wauguzi na madaktari katika kukabili vikwazo vyote na kuzifikia jamii kwa huduma za afya ambazo ni muhimu na za msingi na kusaidia kuchagiza afya bora na lishe ya Watoto na kina mama wajawazito.”

Matatizo ya kiafya

Naibu mwakilishi wa UNICEF nchini Msumbiji Michel Le Penchoux amekumbusha kwamba watoto walio chini ya umri wa miaka mitano na wanawake wajawazito wanakabiliwa na hatari za kiafya na lishe baada ya vimbunga viwili vikumbwa kuikumba Msumbiji, ”wiki ya kampeni ya afya ni hatua muhimu katika kuonga mbele kurejesha huduma za msingi hasa kwa Watoto na wanawake wajawazito walioathirika na kimbunga Idai.”

Naye balozi wa kitaifa wa UNICEF nchini Msumbiji Neymar aliungana na timu ya kiufundi ya shirika hilo kushiriki katika harakati za uelimishaji na kufikisha ujumbe ikiwa ni pamoja na Radio ya taifa ya Msumbiji, Radio za kijamii na matangazo ya kupitia mifumo na majukwaa mbalimbaliili kuelezea umuhimu wa watu kujitokeza na kupatiwa huduma hizi zinazopigiwa upatu katika kampeni.

Changamoto

Kwa mujibu wa UNICEF familia nyingi zinaendelea kurejea kwenye nyumba zao au wanahamia kwenye maeneo salama ambako miundombinu ya msingi na huduma zinahitaji kujengwa upya.

Le Pechoux ameihakikishia Msumbiji kwamba UNICEF imejizatiti kufanya kazi kwa Karibu na wizara ya afya na washirika wengine ikiwemo jamii kuhakikisha kwamba Watoto wote wanapatiwa chanjo na kupewa matone muhimu ya vitamini na lishe itakayosaidia ukuaji wao lkini pia haki yao ya kupata huduma bora za msingi za afya.