Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ebola bado ni mtihani DRC, visa vipya zaidi ya 100:WHO

Wahamasishaji wa kijamii huko DRC kwa usaidizi wa UNICEFwakielimisha jamii kuhusu Ebola.
UNICEF/Mark Naftalin
Wahamasishaji wa kijamii huko DRC kwa usaidizi wa UNICEFwakielimisha jamii kuhusu Ebola.

Ebola bado ni mtihani DRC, visa vipya zaidi ya 100:WHO

Afya

Shirika la afya duniani WHO linasema licha ya kuimarika kidogo kwa hali ya usalama maambukizi ya virusi vya Ebola Kivu Kaskazini na jimbo la Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC yameendelea kushika kasi

Taarifa ya WHO iliyotolewa Alhamisi wiki hii inasema wiki hii pekee viza Zaidi ya 100 vimethibitishwa katika majimbo hayo. Shirika hilo linasema sababu kubwa za kuendelea kusambaa kwa Ebola Kivu Kaskazini na Ituri ni usalama mdogo unaofanya maeneo muhimu kutofikika, jamii kuendelea kutokubali juhudi za kukabili Ebola na kusita kushiriki katika juhudi hizo, kuchelewa kubaini visa vya Ebola na kuchelewa kuwasili kwenye vituo vya tiba ya Ebola.

Hofu ya WHO kuhusu Ebola

WHO inasema moja ya hofu zao kubwa ni idadi ya vifo katika jamii vitokanavyo na visa vya Ebola vilivyothibitishwa au vile vinavyoshukiwa . Idadi hiyo inajumuisha wale waliofariki dunia nyumbani lakini pia wale waliofia kwenye vituo vya afya binafsi au vya umma, hospitali na vituo vya afya vya jamii.

Kwa mujibu wa takwimu za shirika hilo kwa wastani vifo katika jamii ni sawa na asilimia 40 ya visa vilivyoripotiwa kila wiki na idadi inabadilika kila wiki ikiwa ni kati ya wastani wa asilimia 28 hadi 43 ya visa tangu mwanzoni mwa mwezi Aprili mwaka huu baada ya idadi ya juu kabisa iliyoshuhudiwa mwezi Februari ambayo ilikuwa asilimia 71.

WHO inasema katika jumla ya vifo 1147 ambavyo vimeorodheshwa hadi sasa theluthi mbili ya vifo hivyo vimetokea nje ya vituo vya afya na wagonjwa wengi wale wanaowasili vituoni mara nyingi hufika wakati hali imeshakuwa mbaya sana na hufariki dunia mara tu baada ya kulazwa.

Hatari iliyopo

Shirika la WHO linasema vifo hivyo pia ni tishio kubwa la hatari ya maambukizi kwa kuwa wagonjwa walikuwa muda mwingi kwenye jamii kwani dalili bado ni chanzo kikubwa cha maambukizi wakati wa vifo vya watu hao na hata baada ya kufa hususan kwa wana familia na hata wauguzi wa afya vituoni wanakowasili.

Shirika hilo limesisitiza kwamba licha ya kuongezeka kwa visa vya Ebola DRC ni muhimu itambulike kwamba maambukizi hayo yapo Zaidi katika maeneo saba ambayo ni Katwa, Mabalako, Butembo Musienene, Kalunguta na Beni maeneo ambayo kwa ujumla yana asilimia 93 ya visa vyote 350 vilivyoripotiwa  katika siku 21 zilizopita tangu April 24 hadi Mei 14 mwaka huu wa 2019.

Wiki hii pia kisa kimoja kipya kiliripotiwa kwenye kituo cha Alimbongo kikihusishwa na visa vilivyotokea eneo la Katwa.

Changamoto kubwa hivi sasa kwa mujibu wa WHO ni matokeo ya visa ambavyo chanzo chake ni maeneo yaliyoathirika na vinalipuka upya  kwenye maeneo ambayo awali yalikuwa yamefanikiwa kudhibiti maambukizi. Katika kipindi hiki visa vipya vimeripotiwa katika vituo vya afya 91 kutoka katika vituo 18 kati ya 22 vinavyotambulika kuathirika hadi sasa.

Kinachofanyika DRC

WHO na wadau wake wanaendelea na juhudi za kuelimisha na kushirikisha jamii na timu zake ili kufikisha ujumbe kuhusu hatari ya Ebola, maambukizi, na athari zake kwa jamii lakini pia umuhimu wa kupata huduma ya afya mapema kwenye vituo vya afya jambo ambalo litasaidia kuokoa maisha ya wengi.

Ujumbe huu umekuwa na mafanikio hususan maeneo ya Beniambako watu walioambukizwa wanafika kwenye vituo vya afya mara nyingi na mapema Zaidi baada ya kuona dalili.

Inakisiwa kwamba ongezeko la visa litaendelea katika maeneo yaliyoathirika Zaidi na Ebola katika wiki zijazo kufuatia jitihada kubwa za kuanza tena vipimo ili kubaini visa Zaidi na kuvishughulikia.

WHO inasema kuongezeka kwa visa kulikoshuhudiwa hivi karibuni kunadhihirisha bayana hatari ambayo bado ipo ya uwezekano wa kusambaa kwa Ebola katika majimbo ya jirani DRC na nchi jirani.

TAGS:Ebola, DRC, WHO