Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Juhudi za kukabiliana na Ebola DRC zinaendelea

Sampuli za damu zinachunguzwa katika maabara maalum mjini Mbandaka, katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Picha ya WHO/Oka
Sampuli za damu zinachunguzwa katika maabara maalum mjini Mbandaka, katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Juhudi za kukabiliana na Ebola DRC zinaendelea

Afya

Mashirika ya kimisaada   yanayoshughulika  na kukabiliana na mlipuko wa Ebola nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo DRC yanaomba msaada zaidi kuweza kufanikisha juhudi hizo.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoratibu   misaada ya kibinadamu, OCHA, pamoja  na shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM yametangaza pesa zinazohitajika kwa shughuli za kupambana na Ebola DRC.

OCHA imesema inahitaji dola milioni 56.8 huku IOM katika taarifa iliyotoa mjini  Kinshasa, ikiomba dola za kimarekani milioni 1.3.

Tayari imeelezwa kuwa WHO imetoa jumla ya dola milioni 4 kutoka katika fuko la masuala ya dharura, CFE,  ili kufadhili operesheni hizo.

Wakati huo huo, nchini DRC juhudi zinaendelea ili kuhakikisha kuwa mlipuko wa Ebola katika jimbo la Equateur hausambai kwenye majimbo mengine na nchi jirani kama vile  Jamhuri ya Afrika ya Kati.

IOM na WHO kwa ushirikiano na wizara ya afya ya DRC wamelivalia njuga suala hilo ambapo moja ya njia zilizotumiwa kufanikisha azma yao ni kufanya ukaguzi wa sehemu mbalimbali ambazo zinatumiwa kama njia za kuingia na kutoka mji mkuu wa DRC, Kinshasa.

Ukaguzi huu umesaidia jamii kupata uelewa mzuri wa jinsi ya kupanga mikakati ya kuimarisha uchunguzi madhubuti wa kiafya kuzunguka mji mkuu.

Hadi Mei 22 mwaka 2018, watu 27 walikuwa wameripotiwa kufariki dunia huku wengine 58 wamethibitika kuwa wameambukizwa na ugonjwa huo.