Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Operesheni za kukabiliana na Ebola zaanza tena baada ya kusitishwa kwa muda DRC-WHO

Muuguzi akiandaa kitanda kwa ajili ya mtu anayehisiwa kuwa na ugonjwa wa Ebola katika Hospitali ya Bwera, Wilaya ya Kasese karibu na mpaka wa DR Congo.3 September 2018.
UNICEF/UMichele Sibiloni
Muuguzi akiandaa kitanda kwa ajili ya mtu anayehisiwa kuwa na ugonjwa wa Ebola katika Hospitali ya Bwera, Wilaya ya Kasese karibu na mpaka wa DR Congo.3 September 2018.

Operesheni za kukabiliana na Ebola zaanza tena baada ya kusitishwa kwa muda DRC-WHO

Afya

Shirika la afya ulimwenguni, WHO limesema kuwa operesheni za kukabiliana na mlipuko wa ebola kwenye jimbo la Kivu Kaskazini, nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo, DRC  zimeanza tena baada ya kusitishwa kwa muda.

Kwa mujibu wa WHO operesheni za kukabiliana na gonjwa hilo zilikuwa zimeathiriwa na mzozo katika mji wa Beni ambao ni kitovu cha mlipuko wa ebola mwishoni mwa mwezi Desemba mwaka jana.

WHO imesema kufuatia uongozi kutoka kwa serikali na ushirikiano na wadau, operesheni za kukabiliana na ebola zimerejea katika vituo vyote lakini imetoa tahadhari kuwa iwapo kutakuwa na usumbufu wowote huenda ukaathiri hatua zilizopigwa kama kutashuhudiwa vipindi virefu vya ukosefu wa usalama.

Shirika hilo la afya limetaja changamoto kubwa ya harakati za kukabiliana na ebola kuwa ni hali ya usalama, kutoaminiana kwa baadhi ya watu walioathirika na mbinu dhaifu za kuzuia na kudhibiti ebola katika vituo vingi vya umma na binafsi vya afya.

Kufikia sasa visa 625 vimeripotiwa ambapo visa 577 vimethibitishwa na vifo 377 vimeandikishwa tangu mlipuko ulipotangazwa Agosti mwaka jana 2018.

WHO inaripoti kuwa zaidi ya watu 56,500 wamepatiwa chanjo dhidi ya ebola, na watu 220 wamepona.