Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ushiriki wa jamii katika kutokomeza Ebola ni muhimu sana:WHO

 Kikundi cha UNICEF kinachoelimisha wananchi  kuhusu Ebola kinahutubia watu wa Beni Kivyu Kaskazini  mashariki mwa DRC.
© UNICEF/UN0228985/Naftalin
Kikundi cha UNICEF kinachoelimisha wananchi kuhusu Ebola kinahutubia watu wa Beni Kivyu Kaskazini mashariki mwa DRC.

Ushiriki wa jamii katika kutokomeza Ebola ni muhimu sana:WHO

Afya

Shirika la afya ulimwenguni WHO leo limeelezea hofu yake kwa washirika wake wanaochukua hatua pamoja ili kutokomeza Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC kuhusu ushirika wa jamii katika vita dhidi ya ugonjwa huo hatari.

Kwa mujibu wa msemaji wa WHO mjini Geneva Tarik Tsarevic ushirikishwaji wa jamii ni suala la kupewa kipaumbele, “Tumeshuhudia milipuko ikimalizika katika maeneo ambayo jamii zimeshiriki , kuanzia wahudumu wa afya hadi viongozi wa dini na makundi ya vijana. Katika kila mji mpya kulikozuka mlipuko, WHO na washirika wanasayansi ya jamii na wanaanthropojia wanashirikiana na viongozi wa jamii ili kuelewa hali na kuchukua mtazamo ambao utafanya kazi na katika baadhi ya maeneo hilo lilifanya kai haraka.”

Akitolea mfano maeneo ya Beni, ambako awali ilikuwa kitovu cha mlipuko huo wa Ebola Tsarevic amesema licha ya changamoto za ushirika wa jamii hapo mwanzoni mlipuko ulidhibitiwa ndani ya wiki kadhaa lakini maeneo kama Katwa na Butembo bado kuna changamoto.

Tsarevic amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva kwamba timu ya WHO ambayo inafanya kazi kwa Karibu na wiraza ya afya ya DRC na wadau wengine pia imekuwa ikitumia mtazamo mwingine wa majadiliano na jamii.

Na kuongeza kwamba wamekuwa wakijadiliana hususan na wale ambao wana wasiwasi au kukosoa juhudi zinazofanyika na kwa pamoja wanashauriana ni vipi masuala, mahitaji na hofu yao vinaweza kushughulikiwa.

Hata hivyo amesema changamoto ya usalama ya hivi karibuni imeongeza hofu ingawa hakujakuwa na visa vipya kwa siku 21 sasa na asilimia 90 ya watu wanaostahili kupaya chanjo kwa hiyari yao watachanjwa.