Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchi futeni sheria za kibaguzi na muweke za kuwalinda watu wote:UNAIDS

LGBTI wakiwa katika maandamano
OHCHR/Joseph Smida
LGBTI wakiwa katika maandamano

Nchi futeni sheria za kibaguzi na muweke za kuwalinda watu wote:UNAIDS

Haki za binadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na vita dhidi ya UKIMWI, UNAIDS limetoa wito ckwa nchi kote duniani kufuta sheria zote zinazobagua baadhi ya watu kwenye jamii na badala yake kuweka sheria zinazowalinda.

Wito huo umetolewa leo katika kuelekea siku ya kimataifa dhidi ya watu wanaofanya mapenzi ya jinsia moja, waliobadili jinsia na wanaoshiriki mapenzi ya jinsia zote (LGBTI) siku hiyo (IDAHOT) ambayo itaadhimishwa kesho Mei 17.

UNAIDS  inasema sheria za kibaguzi kwa makundi hayo zinawafanya asilimia kubwa ya wasagaji, mashoga , waliobadili jinsia zao, na wanaofanya mapenzi ya jinsia zote (LGBTI) kukosa huduma muhimu za afya na za kijamii.  Ikisisitiza kwamba unyanyapaa dhidi ya kundi hilo la wanaume mashoga  na wanaume wengine wanaofanya mapenzi na wanaume, makahaba, watu wanaojidunga dawa za kulevya, wafungwa, na watu wengine wanaoshikiliwa kuonekana wahalifu. Na hii inachochea machafuko, unyanyasaji, mazingira ya hofu, na  kuwa kikwazo cha juhudi za kufanya huduma ya HIV kupatikana kwa watu wanaoihitaji.


Kwa mujibu wa mkurugenzi mpya mtendaji wa UNAIDS Gunilla Carlsson “Sote tunawajibu wa kimaadili na kisheria kuondoa sharia za kibaguzi na kuweka sharia ambazo zinawalinda watu dhidi ya ubaguzi. Ili kutokomeza janga la ukimwi watu wanahitaji kulindwa dhidi ya madhara, tunahitaji haki na usawa kwa wote.”

Zaidi ya nchi 65 zinaharamisha uhusiano na mapenzi ya jinsia moja ikiwemo angalau 8 ambazo zinatoa hukumu ya kifo kwa videndo hivyo. Kimataifa wanaume mashoga na wanaume wengine wanaoshiriki ngono na wanaume, wako katika hatari mara 28 zaidi ya kupata virusi vya HIV kuliko watu wengine wa kawaida na wana fursa ndogo ya kupata huduma za HIV.

Hali halisi kwa LGBTI

Takwimu za UNAIDS zinaonyesha kwamba kwa mwaka 2017 wanaume mashoga na wanaume wanaoshiriki ngono na wanaume walikuwa ni asilimia 18 ya maambukizi yote mapya ya HIV duniani. Na kwa mantiki hiyo mkurugenzi mkuu wa shirika la afya duniani WHO, Bwana Tedross Adhanom Ghebreyesus amesema “Ni muhimu sana kwamba tunaunda dunia ambayo watu wote wanaweza kupata fursa ya huduma za afya na za kijamii ambazo wanazihitaji bila vitisho vya kukumbwa na ghasia na ubaguzi. Huduma za afya kwa wote inamaanisha kuwafikia watu wote, makundi ya walio wachache ya kijinsia na ushiriki wao wa kingono yana haki sawa kama watu wengine wowote.”

Ameongeza kuwa watu waliobadili jinsia ambao ni sawa na asilimia 0.1-1.1 ya watu wote duniani mara nyingi wanakabiliwa na unyanyapaa, ubaguzi na kukataliwa na jamii majumbani kwao na katika jamii zao. Na vitendo vya ubaguzi, ghasia na uharamishaji vinazuia watu hawa kupata fiursa ya huduma za HIV wanazozihitaji kuwa na afya na inakadiriwa kwamba wanawake waliobadili jinsia wako hatarini mara 13 zaidi kuambukizwa HIV kuliko watu wengine wazima walio katika umri wa kuzaa na kwamba asilimia 16.5 ya wanawake waliobadili jinsia wanaishi na VVU.

Naye mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa maendeleo UNDP , Achim Steiner ameongeza kuwa “Haki na ulinzi kwa wote ni kiini cha kusongesha mchakato wa kufikia ajenya ya 2030 ya maendeleo endelevu  Kuweka na kutekeleza sheria na sera zisizo za kibaguzi , kuondoa sheria zinazotoa adhabu na kuhakikisha fursa ya haki kwa wote ni muhimu kufanikisha ahadi ya kutomwacha yeyote nyuma.”