Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Afrika Kusini na mwelekeo sahihi kupambana na Ukimwi

Muelimishaji rika Arafah akizungumza na kundi la wanafunzi wa shule huku akisambaza vifaa vya kuelimisha kuhusu VVU na Ukimw huko Khartoum, Sudan
UNICEF/SUDA2014-XX166/Noorani
Muelimishaji rika Arafah akizungumza na kundi la wanafunzi wa shule huku akisambaza vifaa vya kuelimisha kuhusu VVU na Ukimw huko Khartoum, Sudan

Afrika Kusini na mwelekeo sahihi kupambana na Ukimwi

AfyaUshahidi zaidi kutoka Cameroon, , Côte d’Ivoire, na Afrika Kusini umezidi kudhihirisha mwelekeo sahihi wa dunia katika kukabiliana na Ukimwi ifikapo mwaka 2020.

Taarifa ya shirika la Umoja wa Mataifa la kukabiliana na Ukimwi, UNAIDS imetolea mfano Afrika Kusini ambayo awali ilikuwa na idadi kubwa zaidi ya watu milioni 7 wanaoishi na virusi vya Ukimwi, VVU na watu milioni 4.4 wanaopata dawa za kupunguza makali ya virusi hivyo.

Tafiti mpya zimeonyesha kuwa hivi sasa nchini Afrika Kusini idadi ya maambukizi mapya ya VVU imepungua kwa asilimia 40 kati  yam waka 2010 na 2017.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS Michel Sidibé akizungumzia ripoti hizo amesema ni muhimu katika kuwezesha nchi kutathmini na kupanga upya mipango yao kuhusu Ukimwi na kuhakikisha watu wanaoishi na VVU wanapata huduma sahihi.

Halikadhalika amesema taarifa hizo mpya zinathibitisha makadirio ya UNAIDS yanayodokeza kuwa Afrika Kusini imepanua wigo wa utoaji wa huduma kwa watu wenye VVU na kufikia lengo la 90-90-90.

Lengo hilo ambalo linapaswa kufikiwa ifikapo mwaka 2020 linamaanisha kuwa asilimia 90 ya watu wenye VVU wafahamu hali yao ya kiafya, asilimia 90 wanaofahamu hali yao ya kiafya wapate matibabu sahihi na asilimia 90 ya wanaopata dawa waweze kupunguza makali ya virusi hivyo ya Ukimwi.

Nchini Afrika Kusini idadi ya watu wanaopima VVU na kutambua hali yao ni asilimia 71 ikiwa ni juu ikilinganishwa na Cameroon na  Côte d’Ivoire ambako ni chini y a asilimia 50.

“Tofauti kubwa kati ya Afrika Kusini na mataifa ya Afrika Magharibi na Afrika ya Kati ni utambuzi wa hali ya VVU ikidokeza kuwa huduma za kupima bado zinapaswa kuimarishwa katika nchi za Afrika ya Magharibi na Kati,” imesema taarifa ya UNAIDS.

Utafiti huu uliongozwa na Chuo Kikuu cha Columbia cha nchini Marekani kwa kushirikiana na serikali husika zikiungwa mkono na mpango wa dharura wa Rais wa Marekani kuhusu Ukimwi, PEPFAR.