Skip to main content

Ukatili shuleni dhidi ya LGBT ni tatizo lilioenea duniani- UNESCO

Ukatili shuleni dhidi ya LGBT ni tatizo lilioenea duniani- UNESCO

Ripoti mpya ya Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), imebainisha kuwa ukatili wa chuki dhidi ya wanafunzi wenye maumbile na mwelekeo tofauti kimapenzi (LGBT) ni tatizo lililoenea kote duniani.

Ripoti hiyo ambayo imetolewa leo katika kuadhimisha siku ya kupinga ubaguzi dhidi ya wapenzi wa jinsia moja na wanaojitambulisha tofauti na muonekano au maumbile yao (IDAHOT), imeonyesha kuwa ailimia 85 ya wanafunzi wa LGBT hukumbana na ukatili wa chuki dhidi yao, na asilimia 45 ya wanafunzi wanaojitambulisha na jinsia tofauti na maumbile yao huacha shule.

Aidha, ripoti hiyo yenye kichwa, Out In The Open, imesema asilimia 33 ya ukatili utokanao na chuki dhidi ya LGBT huwalenga wanafunzi ambao wanadhaniwa kuwa watu wa LGBT kimakosa, kwa sababu muonekano na hulka yao ni tofauti na matarajio ya kilichozoeleka na jamii.

Ripoti inabainisha sura, ukubwa na athari za ukatili utokanao na chuki dhidi ya wanafunzi wa LGBT, jinsi sekta ya elimu inavyokabiliana nao, na mapendekezo ya nini kifanyike katika siku zijazo.