Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali Yemen iko njia panda llicha ya kuondolewa kwa waasi wa Houthi-Griffiths

Luteni Jenerali Michael Lollesgaard alipotembelea bandari za Hodeida, Salif na Ras Issa ili kuona uhamishaji vikosi vya Houthi.
UNMHA
Luteni Jenerali Michael Lollesgaard alipotembelea bandari za Hodeida, Salif na Ras Issa ili kuona uhamishaji vikosi vya Houthi.

Hali Yemen iko njia panda llicha ya kuondolewa kwa waasi wa Houthi-Griffiths

Amani na Usalama

Hali Yemen iko njia panda licha ya kuondolewa kwa waasi wa Houthi kutoka kwenye eneo la bandari la Hodeida ambalo ni muhimu kwa uwasililishaji wa msaada wa kibindamu amesema mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen Martin Griffiths wakati wa kikao cha Baraza la Usalama hii leo juu ya Yemen.

Kuondolewa kwa vikosi vya Houthi kutoka bandari za Hodeida, Salif na Rass Issa kwa usimamizi wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo wa kusaidia utekelezaji wa makubaliano ya Hodeida, UNAMHA ukiongozwa na jenerali luteji Michael Lollesgaard kulifanyika kati ya Mei 11 hadi Mei 14.

Bwana Griffiths ameongeza kuwa, “UNAMHA umethibithisha kwamba Wahouthi waliitoa ushirikiano kikamilifu kuondoka. Vikosi vya Ansar Allah vimeondoka katika bandari tatu za Hodeida, Salif na Ras Issa. Ningependa kumpongeza jenerali na timu yake kwa ushindi.”

Kwa mujibu wa mwakilishi maalum huyo, kuondolewa kwa vikosi hivyo kutaweka mazingira ya Umoja wa Mataifa kusaidia katika usimamizi na ukaguzi wa bandari hizo tatu. Aidha amesema Umoja huo uko tayari kusaidia kuimarisha uzalishaji na utendaji wa bandari ya Hodeida

Aidha bwana Griffiths amepongeza wahouthi kwa kuzingatia makubaliano yaliyofikiwa na serikali ya Yemen mjini Stockholm mwezi Disemba mwaka 2018 na kwa kutangulia kuondoka. Ameongeza kwamba serikali ya Yemen ilikuwa imerejelea dhamira ya kupeleka vikosi vyake tena.

Bwana Griffiths amesema huu ni wakati muhimu lakini ni mwanzo tu na kwamba, “Upelekaji huu wa vikosi ni lazima uambatane na hatua madhubuti na pande zote ili kufikia wajibu wao chini ya makubaliano ya Stockholm,”.

Kwa mantiki hiyo ametoa wito kwa pande husika kwenye mzozo kukubaliana kuhusu mpango wa operesheni kwa ajili ya awamu ya pili ya upelekaji wa vikosi kwa pamoja Hodeida

Licha ya hatua hiyo lakini mwakilishi huyo maalum amesema,”licha ya umuhimu wa matukio ya hivi majuzi, Yemen inasalia katika njia pande, katia ya vita na amani. Wakati kusitishwa kwa mapiganoa Hodeida unazingatiwa , lakini ongezeko la machafuko katika maeneo mengine nchni kote linasikitisha.”

Kwa mujibu wa bwana Grifftihs, hatua madhubuti Hodeida kutawezesha majadiliano kumaliza mzozo. Pia “natumai kwamba pande husika zitaanza majadiliano haraka iwezekanavyo,”

Halikadhalika amesema anamatumaini ya ushiriki wa wanawake katika majadiliano hayo na kuimarishwa kwa ushirki wa wayemen walioko kusini mwa nchi.

Martin Griffiths
UN Photo/Manuel Elías
Martin Griffiths

 

Watu milioni 10 wanategemea msaada wa chakula

Naye Mark Lowcock, Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura, OCHA akihutubia baraza hilo amesema Yemen ni operesheni kubwa zaidi ya huduma za msaada duniani kote hii leo. Akiongeza kwamba, “Hali ya ukame bado inatishia, wayemen milioni 10 bado wanategemea misaada ya chakula kuishi.”

Bwana Lowcock ameongeza kwamba mlipuko wa kipindupindu umeathiri watu 300,000 mwaka huu ikilinganishwa na watu 370,000 mwaka jana 2018. Hatahivyo idadi ya visa vipya inaonekana kupungua katika siku chache zilizopita licha ya kwamba ni mapema kujua kama hali hii itaendelea

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa OCHA changamoto ya hivi sasa ni ufadhili kwa ajili ya misaada ya kibinadamu ambapo kufikia sasa kwa ombi la mwaka huu 2019 kwa ajili ya Yemen limefadhiliwa kwa asilimia 20 tu.

Dunia iko hatarini kukiathiri kizazi kijacho

Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, Henrietta Fore ameliambia baraza hilo kwamba ni muhimu kuongeza juhudi maradufu ili kuunga mkono juhudi za mwakilishi maalum kufikia suluhu la kisiasa ambayo inawaweka watoto kwanza.

Aidha Bi. Fore ameongeza kwamba, “kwa sababu kadri vita vinavyoendelea ndivyo watoto wengi watafariki huku dunia ikitizama. Wakati tunawaangusha watoto hawa, tunaangusha zaidi ya haki zao za msingi, tunaangusha ubindamua wenyewe.”

Mkuu huyo wa UNICEF amehoji iwapo hivyo ndivyo tungependa kuwaangusha watoto akisema, “Hali Yemen ni  mtihani kuhusu utu wetu, na kwa sasa tunafanya vibaya katika mtihani huu, muda unatupa kisogo. Hatutapata fursa nyingine. Watoto milioni 15 nchini Yemen wanatuuliza tuokoe maisha yao. Tafadhali wasaidieni, wanahitaji amani.”

Michael Lollesgaard atoa neno

Luteni Jenerali Michael Lollesgaard ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya ushauri wa zoezi la uondoaji wa majeshi ya Houthi katika mji wa bandari wa Hodeida UNMHA akizungumza na wanahabari kwa njia ya video akiwa Yemen hii leo amesema makubaliano ya Stokhom ya vikosi kuondoka katika bandari yanaendelea vizuri na UNMHA inaendelea kupata nafasi ya kuzifikia bandari.

Vikosi vya Umoja wa Mataifa pamoja na vikosi vya ulinzi wa pwani nchini Yemeni mwishoni mwa juma lililopita vilianza rasmi kufanya doria katika maeneo ya bandari katika mji wa Hudayidah kufuatia makubaliano kati ya majeshi ya Houthi yaliyo chini ya uongozi wa Ansar Allahna na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa kuhusu mkataba wa Hodeida (UNMHA).  

Hatua ya pili ni kuondoka wa vikosi katika eneo la bandari, hali itakayoruhusu kuweza kufikiwa kwa maghala ya vyakula katika bahari  ya shamu.

Luteni Jenerali ameendelea kusema, "nadhani kutoka upande wetu, tunapaswa kujikita zaidi na ilikuwa imepangwa vizuri lakini bado serikali ya Yemeni haijaridhika. Waligundua kwamba hakukuwa na nafasi ya kuthibitisha kinachoendelea, waligundua kwamba hakukuwa na usawa kwamba tunauita umoja kwa sababu walikuwa pia tayari kutekeleza awamu moja. "

Aidha amefafanua kuwa kuna masuala mawili katika awamu ya kwanza, moja ni kuondoa vikosi katika bandari tatu na  pili kuweka mazingira ya watu kufika katika maghala ya bahari ya shamu.