Shehena ya chakula cha msaada Yemen iko hatarini kuoza- UN

Meli Amity ikiwa imetia nanga katika bandari ya Hudeidah Yemen. bandari hiyo ndiyo msaada karibu wote kwa yemen hupitia.
WFP/Fares Khoailed
Meli Amity ikiwa imetia nanga katika bandari ya Hudeidah Yemen. bandari hiyo ndiyo msaada karibu wote kwa yemen hupitia.

Shehena ya chakula cha msaada Yemen iko hatarini kuoza- UN

Msaada wa Kibinadamu

Umoja wa Mataifa umesema suala la la kuyafikia maghala ya shirika la mpango wa chakula duniani, WFP, yaliyohifadhi shehena ya nafaka huko Hudaidah nchini Yemen linazidi kupata umuhimu zaidi kila uchao.

Hiyo ni kwa mujibu wa tamko la pamoja lililotolewa leo na mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen Martin Griffith na mratibu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA Mark Lowcock mjini Geneva Uswisi.

Wamesema shehena hiyo inatosha kulisha watu milioni 3.7 kwa mwezi mmoja lakini wameshindwa kuyafikia maghala yaliyohifadhi chakula hicho kwa zaidi ya miezi mitano sasa, ikielezwa kuwa chakula hicho kiko hatarini kuoza.

 “Tunafurahishwa na ushiriki wa pande zote wa kufanya kazi na Umoja wa Mataifa ili kuweka mazingira muhimu kwa ajili ya kuyafikia maghala bila kuchelewa zaidi. Tunatambua uthibitisho wa Ansar Allah wa kutekeleza makubaliano ya Hudaidah. Tunathamini juhudi zao za mapema kufungua upya barabara za kuelekea kwenye maghala,” amesema Bwana Griffiths.

Aidha Bwana Griffith na Lowcock wamesisitiza kuwa kuhakikisha ufikiwaji wa maghala ni jukumu la pamoja kati ya pande zote zinazohusika katika mgogoro wa Yemen na kuwa kufikiwa kwa maghala hayo kutaufanya Umoja wa Mataifa kuweza kusambaza kwa haraka chakula kwa watu walioko katika uhitaji.

Wakati huo huoUmoja wa Mataifa uko katika mchakato wa kuongeza msaada wa chakula kwa takribani watu milioni 12 kote nchini Yemen ambao wanahangaika kuweza kupata chakula cha kila siku.

TAGS: Hudaidah, Martin Griffith, Mark Lowcock, OCHA.