Ufadhili zaidi bado unahitajika kuinusuru DRC -UN

21 Machi 2019

Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC, ikiwa inaghubikwa na janga la kibinadamu la  muda mrefu duniani, Mkurugenzi mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF Henrietta H.Fore na Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura OCHA, Mark Lowcock leo kwa pamoja wametoa wito wa kuisaidia DRC kufikia mahitaji ya watoto, familia na jamii zilizoko hatarini wakiwemo watu wenye ulemavu, taarifa iliyotolewa mjini Kishasa, New York Marekani na Geneva Uswisi imeeleza.

Taarifa hii ya UNICEF na OCHA inakuja siku chache baada ya wakuu wa mashirika haya kurejea kutoka ziarani nchini DRC. Bwana Lowcock akiongezea kuhusu DRC kuhitaji msaada endelevu wa kimataifa wa kuweka mazingira ya amani na usalama kwa ajili ya maendeleo ya muda mrefu amesema, “makabidhiano ya kisiasa ya amani yanafanyika katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ni fursa ambayo tunapaswa kuitumia. Tunaweza kuushinda mgogoro mkubwa wa kibinadamu na wa muda mrefu. Lakini tunahitaji haraka wafadhili kutoa fedha zaidi kwa kuwa mahitaji yanaendelea kuzizidi uwezo wa rasilimali.” 

Taarifa hiyo imeeleza kuwa pamoja na DRC kupiga hatua katika miaka ya hivi karibuni kwa baadhi ya maeneo, ikiwemo kupungua kwa watoto wanaofariki kabla ya kufikia umri wa miaka mitano na pia idadi kubwa ya watoto waliojiunga shuleni, bado hali ya kibinadamu ni ya kutia shaka. Idadi ya watu wanaokabiliwa na njaa imepanda kutoka watu milioni 7.7 kwa mwaka 2017 hadi kufikia watu milioni 13 mwaka jana. Takribani watoto milioni 4 wana utapiamlo. Kipindupindu, surau na Ebola bado vinachukua maisha ya watu wengi.

Kwa upande wake Bi Fore amesema, “unyafuzi unategemewa kuwashambulia watoto milioni 1.4 walioko chini ya umri wa miaka mitano na kuwaweka katika hatari ya kupoteza maisha. Katika maeneo yaliyoathirika na mgogoro, watoto na vijana wadogo wamechukuliwa na kufanywa wapiganaji, kudhalilishwa kingono na kunyimwa haki ya elimu, afya na ulinzi. Kwa pamoja, jumuiya ya kimataifa na serikali mpya, wanaweza, na wanatakiwa kuwatendea vema watoto.”

Wakiwa mjini Kinshasa, viongozi hao walifanya mazungumzo ya muhimu na rais wa DRC Félix Tshisekedi ambaye alirejelea ahadi ya serikali katika kushughulikia masuala muhimu ya kibinadamu nchini kote. Nao viongozi hao wa Umoja wa Mataifa walieleza mshikamano wa Umoja wa Mataifa kwa watu wa DRC. Pia walikutana na waziri wa afya wa DRC, Oly Ilunga ili kujadili mlipuko wa Ebola na pia magonjwa mengine kama vile surau, kipundupindu na polio ambayo yanaiathiri nchi hiyo.

©MONUSCO/FIB/Mohammed Mkumba
Walinda amani wanawake kutoka Tanzania wanaofanya kazi na kikosi cha kujibu mashambulizi, FIB cha Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo, DRC, MONUSCO katika eneo la Beni, la Mavivi jimbo la kivu Kaskazini DRC.

 

Mjini Goma katika jimbo la mashariki la Kivu Kaskazini, viongozi hao wawili Lowcock na Fore walikitembelea kituo kinachowahudumia na kuwasaidia wanawake wakiwemo manusura wa unyanyasaji wa kingono na kijinsia. Walikutana na manusura wa ubakaji ambao wanapokea matibabu ya kimwili, kisaikolojia na msaada wa kisheria kwa kusaidiwa na UNICEF na wadau wake.

Katika eneo la Bunia, jimbo la Ituri, Lowcock na Fore walitembelea kambi ya wakimbizi wa ndani ambako walikutana na Janette Dusi Lasi ambaye alijeruhiwa na alimpoteza mume wake wakati Kijiji chao kiliposhambuliwa. Hivi sasa anaishi kambini akiwa na watoto wake wanne.

Fore pia alisafiri hadi Beni na Butembo ambako alitembelea vituo vya kupambana na Ebola. Pia alienda katika vituo vya kuwatunzia manusura wa Ebola ambao sasa wana kinga ya virusi hivyo wakiwatunza watoto ambao mama zao wanaendelea na matibabu.

Watoto wanafikia theluthi moja ya visa vyote vya Ebola, idadi kubwa zaidi kuliko milipuko mingine ya awali. Zaidi ya watoto 1000 wametengwa na wazazi wao au wamebakia yatima kutokana na wazazi wao kufariki kwa Ebola.

Mpango wa kusaidia wanadamu nchini DRC kwa mwaka huu wa 2019 unahitaji dola za kimarekani bilioni 1.65 kwa ajili ya kuwasaidia watu milioni 9. Katika kiwango kinachostahili, UNICEF inahitaji dola milioni 326 kufikia mahitaji ya watoto milioni 4.3. Umoja wa Mataifa na washirika wake waliwafikia watu milioni 3.5 nchini humo kwa mwaka jana 2018.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud

Fuatilia Habari: Habari zilizopita za Mada Hii

WFP yakamilisha ugawaji chakula Kongo mashariki kwa wahamiaji 135,000

Shirika la Miradi ya Chakula Duniani (WFP) limeripoti kukamilisha ugawaji wa posho ya siku kumi kwa wahamiaji muhitaji 135,000 ambao waling’olewa makazi kwa sababu ya mapigano.

WHO inajitahidi kudhibiti homa ya Ebola katika DRC ya kati

Shirika la Afya Duniani (WHO) wiki hii limepeleka misaada ya afya ya dharura katika jimbo la mashariki la Kasai Occidental, DRC baada ya kufumka kwa homa maututi ya Ebola katika wiki za karibuni.