Idadi ya nchi zinazotegemea kuuza bidhaa ghafi ili kupata fedha za kigeni zaongezeka- Ripoti

15 Mei 2019

Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa leo imesema idadi ya mataifa ambayo yanategemea bidhaa na mazao ghafi  pekee kwa ajili ya kukuza uchumi wake imeongezeka na kufikia kiwango cha juu zaidi katika kipindi cha miaka 20.

Ikipatiwa jina, Hali ya Utegemezi wa bidhaa yam waka 2019, ripoti hiyo iliyotolewa na kamati ya maendeleo ya biashara ya Umoja wa Mataifa, UNCTAD imesema mataifa hayo ni yale ambayo asilimia 60 ya thamani ya mauzo yake ya nje inatokana na bidhaa.

Idadi ya mataifa hayo imeongezeka kutoka 92 kati ya mwaka 1998 na  2002 na kufikia 102 kati yam waka 2013 na 2017 ambapo.

Akichambua takwimu hiyo, Katibu Mkuu wa UNCTAD Dkt. Mukhisa Kituyi amesema mataifa hayo 102 ni zaidi ya nusu ya mataifa yote duniani ambayo ni 189 akisema, “theluthi mbili kati ya hayo tegemezi ya bidhaa ni nchi zinazoendelea.”

Amesema “kwa kuzingatia kuwa utegemezi wa bidhaa pekee mara nyingi huwa na madhara kwenye uchumi wa taifa, ni muhimu kuchukua hatua za dharura na kupunguza utegemezi huo ili kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu.”

Mataifa  yanayoendelea yameathirika zaidi

Ripoti inaweka bayana kuwa nchi zinazoendelea ndio zinaathirika zaidi kutokana na utegemezi wa bidhaa pekee kwa ajili ya kuuza nje ya nchi.

“Huathiri asilimia 85 ya mataifa yanayoendelea, asilimia 81 ya mataifa yasiyo na fursa ya bahari na asilimia 75 ya mataifa ya visiwa vidogo,” imesema ripoti hiyo wakati ikichambua kiwango cha athari kwa kila nchi.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo eneo lililoathirika zaidi ni nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara ambapo asilimia 89 ya mataifa hayo hutegemea zaidi bidhaa.

Eneo linalofuatia ni Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini ambako asilimia 65 ya nchi za eneo hilo hutegemea kuuza bidhaa nje ili zipate fedha za kigeni.

UNDP
Costa Rica ni miongoni mwa nchi zinazoongoza duniani kwa kuuza mananasi hata hivyo linapoongezwa thamani bei yake inaweza kuwa kubwa zaidi

Utegemezi wa bidhaa ni tatizo sugu

Licha ya taarifa hizo, ripoti inasema kuwa tatizo la kutegemea bidhaa kuuzwa nje ili kuinua uchumi ni tatizo sugu, mataifa yakitegemea mazao ya kilimo na madini.

Msukosuko wa bei umetajwa kuwa chanzo cha mataifa kujikita au kubadili utegemezi wa bidhaa iwe ni madini au mazao.

Ripoti imesema suala mataifa yanayotegemea bidhaa huathiriwa na msukosuko wa bei kupanda na kushuka ikisema kwa wastani bei ya bidhaa kati ya mwaka 2013 na 2017 zilikuwa chini ya kiwango cha miaka ya 2008 hadi 2012.

“Hali hii imesababisha kudorora kwa uchumi katika mataifa 64 yaliyo tegemezi kwenye bidhaa na idadi kubwa zikitumbukia kwenye mkwamo,” imesema ripoti hiyo.

Harakati za kupanua wigo wa bidhaa kupunguza utegemezi

Hata hivyo ripoti imetaja baadhi ya nchi ambazo zimefanikiwa kupanua wigo wa uzalishaji na uuzaji wa bidhaa nje katika kipindi cha miongo miwili iliyopita.

“Mathalani, baadhi ya mataifa yaliyokuwa yanategema kuuza zaidi mafuta nje ya nchi kama vile Oman, Saudi Arabia na Trinidad naTobago, zimeongeza wigo wao wa bidhaa zinazouza nje kwa kuongeza thamani ya bidhaa kwenye uzalishaji,” imesema ripoti.

Mataifa mengine kama Rwanda na Cameroon ambayo yanategemea mafuta au madini yameweza kupanua wigo wa bidhaa zao za kilimo.

Ripoti hii ambayo ni ya nne tangu kuanza kuzinduliwa mwaka 2012, ina takwimu za mataifa 189.

FAO/Franco Mattioli
Ng'ombe wanaofugwa katika mabanda wakila nyasi

Baraza Kuu lajadili hatua kuondokana na uuzaji wa mazao na bidhaa ghafi

Kuelekea uzinduzi wa ripoti hiyo, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limekuwa na mjadala kuhusu masoko  ya bidhaa ambapo washiriki wamepigia chepuo mabadiliko ya sera ili kuhakikisha kuwa mataifa yanaongeza thamani kwenye mazao  yao badala ya kuyauza yakiwa ghafi. 

Mathalani Mario Cimoli,  ambaye ni Naibu Katibu Mtendaji wa Tume ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa kwa nchi za Kusini mwa Amerika na na Karibea akiwasilisha mada kwenye mkutano huo amesema mataifa ya ukanda huo yanazalisha kwa kiasi kikubwa madini aina ya Lithium hata hivyo hayanufaiki vya kutosha kwa kuwa bei ya Lithium ghafi inakuwa ni ya chini kwenye soko la dunia kwa hiyo ni vyema kusaka mbinu za kushirikiana na kampuni zinazotengeza betri ili kuona jinsi ya kuongeza thamani na hivyo kuongeza bei ya bidhaa hiyo.

Mwakilishi wa Malawi kwenye mkutano huo  akichangia mada amesema ni kweli mada ya masoko ya bidhaa imekuja wakati muafaka na ni vyema kuangalia ni kwa jinsi gani wakulima wanaweza kusaidiwa pindi kunakuwepo na msukosuko wa bei za bidhaa.

Amependekeza uwepo wa mifumo ya bima ambayo itasaidia kufidia hasara ambayo wakulima wanapata pindi bidhaa zao zinaposhuka bei.

 

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter