Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uwekezaji ni muarobaini wa kufanikisha SDGs- Kituyi

Uwekezaji madhubuti katika miundombinu baina ya nchi utasaidia kuboresha biashara na kuinua uwezo wa viwanda barani Afrika. Picha: UM

Uwekezaji ni muarobaini wa kufanikisha SDGs- Kituyi

Ukuaji wa Kiuchumi

Kulikoni wawekezaji wa kigeni sasa hawana tena moyo wa kuwekeza katika nchi duniani hususan zile zinazoendelea?

Wawekezaji wa kigeni wanasuasua kuwekeza katika nchi hususan zilizoendelea na hivyo kuweka mashakani mafanikio ya malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

Katibu Mkuu wa kamati ya biashara na maendeleo ya Umoja wa Mataifa, UNCTAD Dkt. Mukhisa Kituyi amesema hayo jijini New York, Marekani kando mwa mkutano ulioangazia uchangishaji wa fedha kwa ajili ya maendeleo, akitaja miongoni mwa sababu za kusuasua kwa wawekezaji hao.

Ametaja sababu hizo kuwa ni pamoja na nchi zinazoendelea kupenda miradi ya maendeleo lakini maandalizi yake hayafikii kiwango cha kushawishi wawekezaji kupeleka fedha zao.

Sababu nyingine ni hali ya kisiasa ambayo Dkt. Kituyi amelinganisha na dhoruba ya kibiashara ambayo inasababisha hofu, shaka na shuku kwa wawekezaji na pia kule ambako miradi inapelekwa. Dkt. Kituyi ametaja pia baadhi ya viongozi wa kisiasa bado hawajaona uhusiano wa vitegauchumi vya kigeni nchi mwao, FDIs na malengo ya maendeleo endelevu SDGS.

Kwa mantiki hiyo amesema wameandaa kikao maalum kando mwa mjadala wa ngazi ya juu wa viongozi mwezi Septemba mwaka huu jijini New York, ambapo viongozi watakaohudhuria watapata fursa ya kuhamasishwa kuhusu uhusiano huo.