Skip to main content

Sasa uwekezaji haungalii ujira mdogo bali utayari wa kiteknolojia- UNCTAD

Teknolojia  kama nyenzo.
ITU
Teknolojia kama nyenzo.

Sasa uwekezaji haungalii ujira mdogo bali utayari wa kiteknolojia- UNCTAD

Ukuaji wa Kiuchumi

Ripoti mpya ya mwaka 2018 kuhusu uwekezaji wa moja kwa moja wa vitegauchumi ugenini, FDI,  imeonesha kuporomoka kwa uwekezaji na ikiwa ni mwaka wa tatu mfululizo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo, Katibu Mkuu wa kamati ya biashara na maendeleo ya Uomja wa Mataifa, UNCTAD, Dkt. Mukhisa Kituyi amesema anguko la mwaka 2018 ni kwa asilimia 13 duniain kote na kufikia thamani ya dola trilioni 1.3

Dkt. Kituyi amesema ingawa kuna tofauti kati ya eneo na eneo, lakini kwa nchi zinazoendelea barani Ulaya, kiwango cha kupungua kwa FDI kilikuwa ni kikubwa akitolea mfano Uingereza ambayo kiwango cha uwekezaji wa kigeni kilipungua kwa asilimia 36 mwaka 2018.

Sababu kubwa ya anguko hilo kwa mujibu wa Dkt. Kituyi, ni mabadiliko ya sera za kodi nchini Marekani akisema kuwa, “kampuni kubwa za kimataifa ziliamua kurejesha uwekezaji nchini Marekani kutokana na marekebisho ya mfumo wa kodi.”

Anguko la FDI Ulaya laleta nuru Afrika, Kenya kidedea

Hata hivyo amesema kupungua kwa vitegauchumi kwa nchi zilizoendelea kulikuwa ni ‘kivuno’ kwa nchi zinazoendelea ambapo asilimia 50 ya FDI kwa mwaka 2018 zilielekezwa nchi zinazoendelea.

“Uwekezaji wa kigeni barani Afrika uliongezeka kwa asilimia 11, ukichangiwa na kuendelea kuimarika kwa chumi kubwa barani humo kama vile Misri na Nigeria katika miaka iliyotangulia, lakini zaidi kurejea kwa hali nzuri Afrika Kusini baada ya kudorora kwa muda mrefu,” amesema Katibu Mkuu huyo wa UNCTAD.

Ameongeza kuwa maendeleo ya uwekezaji kwenye sekta ya huduma ya teknolojia ya habari na mawasiliano, ICT yamechangia kuongezeka kwa FDI barani Afrika akitaja Kenya kuwa mstari wa mbele na mnufaika.

Kuhusu nchi za Asia zinazoendelea, Dkt. Kituyi amesema zimeendelea kuwa mpokeaji mkubwa wa FDI ambapo katika kipindi cha mwaka 2018 huku kwa nchi za Amerika ya Kusini, kiwango kimepungua zaidi ikiwa ni chini ya asilimia 27.

 Ujira mdogo si kichocheo cha uwekezaji, bali sasa ni utayari kiteknolojia

Dkt. Kituyi ameonya kuwa ni lazima ifahamike vichocheo vya kuporomoka kwa FDI si vya muda mfupi, akitaka mvutano katika suala la teknolojia hasa kwenye biashara, akisema hivi vitadumu kwa muda mrefu.

Halikadhalika amesema mazoezi ya kwamba kwenye vitegauchumi vitapelekwa zaidi katika nchi ambamo ujira kwa wafanyakazi ni mdogo, sasa yamepitwa na wakati kwa kuwa kampuni kubwa zinaelekea vitagauchumi kule ambako nchi zimejiandaa vyema kiteknolojia.

Ripoti ya FDI imekuwa ikitolewa tangu mwaka 1999, ambapo mwaka huu imechunguza pia vichocheo vya uwekezaji wa kigeni, kanuni, sheria na mifumo ya utawala kwenye sekta ya fedha na uwekezaji.